Hali ya kisiasa Burundi yatia matumaini- Kafando
Mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa Burundi, Michel Kafando amesema hali ya kisiasa nchini humo imeanza kutia matumaini wakati huu ambapo taifa hilo linajiandaa kufanya uchaguzi mkuu hapo mwakani.
Bwana Kafando amesema hayo leo mjini New York, Marekani wakati akihutubia wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa waliokutana kujadili Burundi na kupokea taarifa ya Katibu Mkuu kuhusu taifa hilo la Maziwa Makuu.
Ametolea mfano hatua iliyotajwa ya aina yake ya kusajiliwa tarehe 14 mwezi huu kwa CNARED, ambacho ni chama cha upinzani kinachoongowa na Agathon Rwasa, hatua ambayo itawezesha chama hicho kushiriki kwenye uchaguzi mkuu mwakani.
Bwana Kafando amesema hatua hiyo pamoja na ile ya Rais Pierre Nkurunzinza ya kurejelea tena mwezi Disemba mwaka jana kuwa hatowania tena nafasi ya urais wakati wa uchaguzi mkuu mwakani, ni ishara dhahiri ya kupanuka kwa uwanja wa demokrasia nchini humo.
Mazungumzo kati ya warundi
Kuhusu mazungumzo kati ya warundi ambayo yalivunjika, Bwana Kafando amesema kinachofanyika sasa anafuatilia mfumo mpya ambao kwao utaongozwa na marais wa Tanzania, Kenya na Uganda ili afahamu kwa kina yanachukua mwelekeo upi.
Hata hivyo amempongeza Rais mstaafu wa Tanzania Benjamin Mkapa ambaye alikuwa msuluhisho wa mzozo wa Burundi.
Hata hivyo amesema mwelekeo utatia matumaini zaidi iwapo mazungumzo kati ya warundi yatafanyika kwa uwazi akisema kuwa, atawasiliana na marais wa Kenya, Tanzania na Uganda “ili nifahamu mfumo mpya waliokubaliana juu ya mchakato huo mpya wa mazungumzo”.
Mjumbe huyo maalum wa wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa Burundi akatoa wito kwa wajumbe wa Baraza la Usalama ya kwamba iwapo watataka kutoa taarifa yoyote ile kuhusu taifa hilo, “chonde chonde ungeni mkono harakati za ukanda huo za kusaka suluhu Burundi. Ni muhimu usuluhishi huo upatie kipaumbele suala la ujumuishi, ambalo litatoa hakikisho la suluhu ya kudumu kwa mujibu wa makubaliano ya Arusha na kufanyika kwa uchaguzi huru na wazi mwaka 2020.”
AU nasi bado tuko bega kwa bega na Burundi
Akihutubia kikao hicho, Mwakilishi Maalum wa Muungano wa Afrika kwenye Umoja wa Mataifa, Fatima Kyari Mohammed naye ameunga mkono kuwepo kwa utulivu kwenye hali ya siasa nchini humo kuelekea uchaguzi mkuu mwakani.
Hatua hiyo ni pamoja na kuanzishwa kwa tume huru ya taifa ya uchaguzi.
Hata hivyo kwa upande wa hali ya kibinadamu amesema inatia changamoto kwa kuzingatia kuwa ingawa kuna wakimbizi wako tayari kurejea nyumbani kutoka kambini nchini Tanzania, bado wana shaka na shuku juu ya mustakabali wao wanaporejea.
Tume ya ujenzi wa amani ya Burundi
Naye Mwenyekiti wa Tume ya ujenzi wa amani ya Burundi Balozi Jiirg Lauber amepongeza hatua ya serikali ya nchi hiyo kutia saini na Umoja wa Mataifa mpango wa usaidizi wa maendeleo, UNDAF kwa mwaka 2019-2023.
Hata hivyo amesihi mashauriano zaidi yaendelee na wadau wa kimataifa ili kuweza kuanza kufadhili miradi hiyo ya maendeleo kwa maslahi ya wananchi.
Hoja ya Burundi kwenye Baraza la Usalama haina tena mashiko- Balozi Shingiro
Kisha iliwadia fursa kwa Mwakilishi wa kudumu wa Burundi kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Albert Shingiro kuhutubia wajumbe wa Baraza la Usalama ambapo alisema ni dhahiri shairi kuwa kuna maendeleo makubwa katika mchakato wa kisiasa nchini Burundi akisema kuwa serikali imeanzisha mifumo ya kuhakikisha uchaguzi mkuu unafanyika kwa amani na utulivu, sambamba na Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi ambayo tayari inafanya kazi.
Halikadhalika amesema tayari kuna mazungumzo baina ya vyama vya upinzani kwa mujibu mwa utaratibu wa Kayanza na kwamba Burundi imejizatiti kuliko wakati wowote ule kusongesha haki za binadamu.
Mazungumzo baina ya warundi mtuachie wenyewe
Kuhusu mazungumzo kati ya warundi, Balozi Shingiro amesema, “ujumbe wangu unapenda kusisitiza kuwa mazungumzo ni utamaduni na tabia ya kipekee inayoendana na maisha ya warundi. Kwa hiyo si muhimu tena kwa wadau wan je kujionyesha kuwa wao ni viongozi wa mchakato huo ambao ni wa kwetu.”
Akatamatisha hotuba yake kwa kurejelea kile alichosema ni kaulimbiu yake kwa Baraza la Usalama ya kwamba liondoe hoja ya Burundi kwenye ratiba yake, “kwa sababu hali ya Burundi si tishio kwa amani na usalama duniani. Hali ya kisiasa na kiusalama haina kitisho na niwaeleze kuwa uwepo wa vikao vya mara kwa mara kwa mujibu wa azimio namba 2303 kuhusu Burundi kunaleta zaidi ukosefu wa amani kuliko amani.”
Balozi Shingiro amesema kwa miaka minne sasa kuna nchi ambazo zinasisitiza kuwa hoja hiyo iendelee kuwepo lakini, “ni wakati wa wadau hao waondokana na fikra hizo.”