Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yaungana na Kenya kutatua suala la kambi za Dadaab na Kakuma

Kambi ya wakimbizi ya Dadaab kaskazini mwa Kenya ina idadi ya wakimbizi zaidi ya 200,000 na wanaotafuta hifadhi.
UNHCR
Kambi ya wakimbizi ya Dadaab kaskazini mwa Kenya ina idadi ya wakimbizi zaidi ya 200,000 na wanaotafuta hifadhi.

UNHCR yaungana na Kenya kutatua suala la kambi za Dadaab na Kakuma

Wahamiaji na Wakimbizi

Kufuatia hivi karibuni serikali ya Kenya kutangaza nia ya kuzifunga kambi za wakimbizi za Kakuma na Dadaab zinazowahifadhi wakimbizi na wasaka hifadhi takribani 430,000, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNCHR, kupitia taarifa iliyotolewa hii leo mjini Geneva Uswisi, limetangaza kushirikiana na Kenya na kuweka mapendekezo ya hatua za kuchukua ili kupata suluhisho kwa wakimbizi wanaoishi katika kambi hizo.  

Ili kuelekea katika suluhisho endelevu, UNHCR imesema, kwa kushirikiana na serikali ya Kenya watachukua hatua ikiwemo kuboresha urejeaji wa hiari kwa usalama na hadhi huku wakizingatia vizuizi vya kutembea vinavyohusiana na janga la COVID-19 linaloendelea.  Kuweka mipango mbadala ya wakimbizi wanaotoka katika nchi za Afrika Mashariki kuweza kubaki na hii ikimaanisha kuwapa fursa kubwa wakimbizi kuweza kujitegemea na kuchangia katika uchumi wa eneo husika. Kuongeza kasi ya kutolewa kwa vitambulisho vya kitaifa kwa zaidi ya Wakenya 11,000 ambao hapo awali walitambuliwa kama waliosajiliwa katika hifadhi ya data za wakimbizi, na kuendelea kwa mchakato wa uhakiki kwa wengine walioko katika hali kama hizo na pia kuhamishiwa katika nchi za tatu wakimbizi wachache ambao hawawezi kurudi katika nchi zao na wanakabiliwa  na hatari za ulinzi. 

"Tumesikia wasiwasi uliooneshwa na Serikali ya Kenya na tunatumaini kuwa hatua hizi zitakuwa hatua muhimu katika kuharakisha suluhisho endelevu kwa wale wote wanaohusika." amesema Fathiaa Abdalla, Mwakilishi wa UNHCR nchini Kenya. 

Aidha afisa huyu wa UNHCR amesema, “tunaamini kwamba kupitia hatua mpya za pamoja tunaweza kuweka hatua zinazoheshimu haki za wakimbizi na kusababisha suluhisho endelevu. Tunatarajia kuendelea na mazungumzo na ushirikiano wetu na mamlaka na washirika wa Kenya juu ya jambo hili muhimu. "