Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ajira na maisha bora vimetushawishi kurejea nyumbani:Wakimbizi wa Kisomalia

Kundi la wanawake mjini Mogadishu Somalia.
OCHA
Kundi la wanawake mjini Mogadishu Somalia.

Ajira na maisha bora vimetushawishi kurejea nyumbani:Wakimbizi wa Kisomalia

Amani na Usalama

Maelfu ya wakimbizi wa Somalia walioko katika kambi za wakimbizi za Dadaanb na Kakuma nchini Kenya wanakata shauri na kuamua kurejea nyumbani wakiwa na matumaini ya kupata kazi na Maisha bora . Jason Nyakundi na taarifa zaidi

Kwa mujibu wa taarifa ilitolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, kambi ya Dadaab ambayo ilikuwa na wakimbizi wa Kisomali zaidi ya 466,000 mwaka 2011 hivi sasa kufuatia mpango wa hiyari wa wakimbizi kujerea nyumbani  na pia baadi ya wakimbizi kukata shauri wenyewe kutaka kurudi nyumbani idadi ya wakimbiz wa Kisomali imepungua na kufikia 210,498.

Miongoni mwa wakimbizi hao waliokata shauri ni Bi. Fatuma Abdi Rahman mtaalamu wa kupaka hina na mama wa watoto watatu anasema “ninaamini kwamba nitaweza kuisaidia familia yangu nikirejea tena nyumbani Kismayo baada ya kutengana na mume wangu wanangu wananihitaji sasa kuliko wakati mwingine wowote. Ingawa shule Kismayo sio bure kama hapa Dadaab lakini natarajia kuendelea na biashara ya hina na kuwalipia wanangu karo ya shule.”

Hayo ni matumaini ya wakimbizi wengi wa Kisomali kwani ajira na maisha bora ndiuo wanachokisaka. Mkataba wa kuwarejesha nyumbani wakimbizi kwa hiyari ulitiwa saini n apande tatu 2013 kati ya serikali ya Kenya, serikali ya mpito ya Somalia na UNHCR na katika awamu ya majaribio zaidi ya wakimbizi 2,588 walisaidiwa kurejea Kismayu, Baidoa na Luug, na baada ya kufanikiwa maeneo mengine  yameongezwa na sasa ni 12 ikiwemo Moghadishu.

UNHCR inashirikiana na na wadau wengine wa kimataifa likiwemo baraza la wakimbizi la Denmark na shirika la Save the children katika kufanikisha mchakato huu. UNHCR inaamini kwamba baada ya miaka 28 ya kambi ya Dadaab kuna haja ya kusaka suluhu ya kudumu kwa wakimbizi wa kambini hapo na mojawapo iliyo endelevu ni kuwarejesha nyumbani kwa hiyari.

Leo kuna wakimbizi zaidi ya 2,000 ambao wamejiandikisha kwa hiyari kurejea Kismayo, Baidoa na Moghadishu. Kuna Jumla ya wakimbizi wa Kisomali 809,273 Afrika Mashariki na kati yao takriban 260,000 wako kwenye kwenye kambi za Dadaab, Kakuma na wengine maeneo ya mijini.