Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR na Kenya zakubaliana kuhusu mustakabali wa kambi za Kakuma na Dadaab

Wakimbizi wapanga foleni kupokea mgao wa chakula katika kambi ya Kakuma Kaskazini mwa Kenya.
WFP
Wakimbizi wapanga foleni kupokea mgao wa chakula katika kambi ya Kakuma Kaskazini mwa Kenya.

UNHCR na Kenya zakubaliana kuhusu mustakabali wa kambi za Kakuma na Dadaab

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR na serikali ya Kenya wamekubaliana juu ya mustakabali wa kambi za wakimbizi za Kakuma na Dadaab nchini humo kwa kuridhia kuunda kamisheni ya pamoja ya kutoa majawabu ya masuala ya msingi kuhusu hatma ya wakimbizi.

Hatua hiyo inafuatia mazungumzo ya pamoja kati ya Kamishna Mkuu wa UNHCR Filippo Grandi na Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, mazungumzo yaliyofanyika Ikulu jijini Nairobi Kenya siku ya Alhamisi, mazungumzo yaliyofanyika kufuatia tangazo la Kenya la nia yake ya kuzinguza kambi hizo za wakimbizi.

Yaliyokubaliwa kati ya UNHCR na Kenya

Taarifa ya pamoja iliyotolewa mwishoni mwa mazungumzo hayo inasema "jopo la pamoja likiwa n maafisa kutoka serikali ya Kenya na UNHCR litaundwa ili kukamilisha na kutekeleza mpango wa hatua za kuchukuliwa ili kushughulikia kwa utu wakimbizi katika kambi hizo mbili."

Mpango huo uliwasilishwa kwa serikali ya Kenya mwanzoni mwa mwezi huu wa Aprili na unajumuisha wakimbizi kurejea kwa hiari nyumbani kwa utu na kwa usalama, wakimbizi kupelekwa nchi ya tatu na kupata makazi na mpango mbadala wa kusalia nchini Kenya kwa baadhi ya wakimbizi kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC.

Maafisa wa serikali walioshiriki mkutano huo ni pamoja na Fred Matiang’i ambaye ni Waziri wa Mambo ya Ndani ambaye amesema "tuko makini sana kuhusu kukamilisha mpango wa kuwarejesha wakimbizi nyumbani ulioanza mwaka 2016, kwa kuzingatia wajiu wetu wa kimataifa na wajibu wetu hapa nchini. Kwa hiyo tunasisitiza msimamo wetu wa awali wa kufunga kambi zote mbili yaani Dadaab na Kakuma ifikapo tarehe 30 mwezi Juni mwaka 2022."

Mama akimlisha mtoto wake mwenye utapiamlo katika kliniki ya Madaktari wasiokuwa na mipaka katika kambi ya Dadaab, Kenya.
OCHA/Meridith Kohut
Mama akimlisha mtoto wake mwenye utapiamlo katika kliniki ya Madaktari wasiokuwa na mipaka katika kambi ya Dadaab, Kenya.

Kambi si suluhu ya kudumu, tufazifunga ifikapo Juni 30 2022

UNHCR na serikali ya Kenya wamekubaliana kuwa "kambi za wakimbizi siyo suluhu la kudumu katika tatizo la ukimbizi na watu kufurushwa makwao, na tumeazimia kushirikiana ili kusaka suluhu mbadala kwa mujibu wa misingi tuliyokubaliana pamoja na maengo ya mkataba wa wakimbizi, GCR", imesema taarifa hiyo ya pamoja.

Kwa upande wake, Kamishna Mkuu Grandi amesema "naamini serikali ya watu wa Kenya wataendelea kuonesha ukarimu wao kwa wakimbizi kama walivyofanya kwa miongo takribani mitatu, huku tukiendelea na majadiliano ya mkakati wa kusaka suluhu ya kudumu, sahihi na inayozingatia haki za wakimbizi na wasaka hifadhi kwenye kambi za Dadaab na Kakuma."

"Kufungwa kwa kambi lazima kuonekane kuwa ndio lengo. Hatufukuzi watu, lakini kambi siyo suluhu ya kudumu. Ni pahala pa sintofahamu. Hakuna mtu anapaswa kuishi maisha yasiyo ya uhakika au utu kizazi baada ya kizazi. Tunachoshughulikia sasa ni jinsi ya kufanikisha hilo kwa ushirikiano na kwa mujibu wa mkataba wa kimataifa kuhusu wakimbizi.," amesema Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Balozi Raychelle Omamo ambaye naye alishiriki mazungumzo hayo.

Tweet URL

Grandi amekaribisha hatua ya Kenya ya kuendelea kufanya kazi kwa kuzingatia mkataba huo wa kimataifa wa wakimbizi akisema, "nina uhakika kutokana na hakikisho la serikali kuwa wataendelea kupatia wakimbizi na wasaka hifadhi huduma na ulinzi wakati suluhu nyingine zinaendelea kutafutwa."

Makubaliano yaliyofikiwa

Miongoni mwa yaliyomo kwenye mpango wa serikali ya Kenya ni azimio lililopitishwa kwa kauli moja na mawaziri na wawakilishi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC zenye uhusiano wa kibalozi na Kenya pindi walipokutana na ujumbe ulioongozwa na Dkt. Matiang’i.

Pande hizo zilikubaliana kuwa wakimbizi kutoka nchi wanachama wa EAC watapatiwa fursa ya kupatiwa vibali vya kazi bila gharama yoyote ili waweze kujumuika katika jamii ya Kenya au warejee nchi zao za asili.

Utambuzi wa kidijitali wa wakenya ambao pia wamesajiliwa kama wakimbizi unatarajiwa kuanza hivi karibuni. Hatua hii itatoa fursa ya kupatia vitambulisho sahihi raia wa Kenya na kuhakikisha wanatolewa kwenye kanzi data ya wakimbizi.

Kenya imekuwa inahifadhi wakimbizi kwa takribani miongo mitatu sasa na hivi sasa kambi hizo zimezidiwa uwezo.

Serikali ya Kenya imekuwa inaelezea wasiwasi wake juu ya ukosefu wa usalama kwa wakenya na wakimbizi huko kambini ambako kwa sasa kambi zote mbili zinahifadhi jumla ya wakimbizi 433,765.