Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uhusiano kati ya kuvia damu na chanjo ya AstraZeneca wawezekana lakini haujathibitishwa- WHO

Chanjo ya AstraZeneca/Oxford dhidi ya COVID-19 inatengenezwa nchini India chini ya leseni maalum.
© UNICEF/Dhiraj Singh
Chanjo ya AstraZeneca/Oxford dhidi ya COVID-19 inatengenezwa nchini India chini ya leseni maalum.

Uhusiano kati ya kuvia damu na chanjo ya AstraZeneca wawezekana lakini haujathibitishwa- WHO

Afya

Kamati ndogo ya kamati ya kimataifa ya kushauri shirika la afya la Umoja wa Mataifa ulimwenguni, WHO, kuhusu usalama wa chanjo imesema uhusiano wa binadam kuvia damu baada ya kupatiwa chanjo ya AstraZeneca unawezekana kuwepo lakini bado kuthibitishwa.

 

Kamati hiyo imetoa uamuzi huo wa muda baada ya kikao chake cha leo tarehe 7 mwezi Aprili, ikisema uamuzi huo wa muda unafuatia taarifa kutoka mamlaka ya dawa ya Ulaya, Uingereza na mamlaka ya udhibiti wa dawa, MHRA  na nyingine wanachama wa WHO.

Taarifa ya kamati hiyo imesema, “kwa kuzingatia taarifa zilizopo sasa, uhusiano kati ya chanjo ya AstraZeneca na anayepatiwa chanjo hiyo kuvia damu unawezekana kuwepo lakini haujathibtishwa. Tafiti mahsusi zinatakiwa kufanyika ili kufahamu kwa kina uhusiano kati ya chanjo na hatari zinazoweza kutokea.”

Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa Geneva, Uswisi,  kamati hiyo ndogo itaendelea kukusanya na kupitia taarifa, kadri ambavyo imekuwa ikifanya tangu kuanza kutolewa kwa chanjo.

“Ni muhimu kutambua kuwa ingawa zinatia wasiwasi, matukio hayo ya damu kuvia bado ni machache, ambapo ni watu wachache wameripotiwa miongoni mwa watu milioni 200 ambao wamepokea chanjo ya AstraZeneca duniani kote,” imesema taarifa hiyo.

Cambodia ikipokea dozi 324,000 za AstraZeneca dhidi ya COVID-19 kupitia mkakati wa chanjo wa COVAX
© UNICEF/Antoine Raab
Cambodia ikipokea dozi 324,000 za AstraZeneca dhidi ya COVID-19 kupitia mkakati wa chanjo wa COVAX

Madhara baada ya chanjo ni kawaida, dalili zikizidi muone daktari

Taarifa hiyo imeongeza kuwa matukio machache ya madhara baada ya kupatiwa chanjo yanapaswa kutathminiwa dhidi ya hatari ya vifo vya coronavirus">COVID-19 vinavyoweza kutokea, na uwezekano wa chanjo hiyo kuzuia maambukizi na kupunguza vifo kutokana na ugonjwa huo. Ni kwa mantiki hiyo “inapaswa kutambuliwa kuwa hadi leo hii Jumatano, takribani watu milioni 2.6 wamefariki dunia kutokana na coronavirus">COVID-19 duniani kote.”

Halikadhalika imesema kuwa madhara yatokanayo na chanjo siku mbili au tatu baada ya mtu kupatiwa chanjo, hutarajiwa na kwa kiasi kikubwa madhara hayo si makubwa.

Hata hivyo taarifa hiyo imesema, “mtu anayepata dalili kali zaidi kama vile kushindwa kupumua, maumivu ya kifua, kuvimba miguu, maumivu ya tumbo yasiyokwisha, maumivu ya kichwa na kushindwa kuona vizuri, sambamba na alama za kuvia damu kwenye ngozi zaidi ya pale alipodungwa chanjo, kati ya siku 4 hadi 20 baada ya chanjo anapswa kumuona daktari.”

Kamati hiyo ndogo ya ushauri imesema wahudumu wa afya wanapaswa kutambua dalili hizo ipasavyo zinazoweza kutokea pindi mtu anapatiwa chanjo dhidi ya Corona. Ni kwa mantiki hiyo kama hiyo imedokeza kuwa kamati ya wataalamu wakiwemo wale wa masuala yad amu ikutane ili itoe ushauri juu ya uchunguzi wa kitabibu na ushughulikiaji wa hali hiyo.

Kwa upande wake WHO imesema inaendelea kufuatilia kwa kina usambazaji wa chanjo dhidi ya Corona, na itaendelea kushirikiana nan chi katika kusimamia hatari zinazoweza kutokea na kutumia sayansi na takiwmu kuchukua hatua na kutoa mapendekezo.