Chanjo ya Johnson & Johnson ruksa kutumika licha ya hofu ya kuganda kwa damu:WHO

17 Machi 2021

Chanjo ya Janssen  dhidi ya virusi vya COVID-19  leo imeidhinishwa hadharani kwa matumizi ya kimataifa na bodi ya ushauri ya wakala wa afya wa shirika la Umoja wa Mataifa SAGE, ambayo pia imeondoa wasiwasi wa kuganda kwa damu kunakohusishwa na nchi zingine dhidi ya chanjo za COVID-19 , bila kuwa ushahidi dhahiri

Katika mkutano na waandishi wa habari Geneva Uswis, SAGE imesifu kipimo cha dozi moja ya chanjo ya Janssen iliyotengenezwa na kampuni tanzu ya Johnson & Johnson kuwa ni salama na ni nyongeza nyingine ya kuokoa maisha kwa chanjo zingine tatu ambazo tayari zimepitishwa kutumika za Pfizer, Moderna na AstraZeneca.

Jopo la wataalam hao pia limebaini kuwa matukio ya kuganda kwa damu  ambayo yanajulikana pia kama hypercoagulable ilikuwa ni dalili ya COVID-19, wakati ziliposimamishwa chanjo ya AstraZeneca / Oxford na nchi kadhaa za Ulaya, ikisubiriwa tathimini ya kisayansi.

Hizi ni bidhaa zinazookoa maisha

“Ulimwengu uko mahali ambapo hakuna ugavi wa kutosha kukidhi mahitaji ya watu wanaohitaji chanjo, ni wazi kwamba chanjo yoyote kati hizi ni bidhaa zinazookoa maisha” amesema Dakt. Kate O'Brien, mkurugenzi, idara ya chanjo, na Biolojia katika Shirika la afya  la Umoja wa Mataifa (WHO).

Amesisitiza kuwa chanjo "zinahitaji kutumiwa haraka iwezekanavyo kadri zinavyopelekwa. Watu wanaweza kuwa na imani na usalama, ufanisi na ubora wa utengenezaji wa bidhaa hizo. "

 

Utafiti na majaribio yanaendeshwa kote duniani kwa ajili ya kupata chanjo mbalimbali za COVID-19
Jannsen
Utafiti na majaribio yanaendeshwa kote duniani kwa ajili ya kupata chanjo mbalimbali za COVID-19

Wakati wa majaribio ya chanjo ya Janssen iliyohusisha karibu watu 44,000, watu 10 kati ya kundi la kwanza la watu 22,000 waliopata dozi ya chanjo hiyo walipata tatizo la kuganda kwa damu wakati 14 kati ya 22,000 waliochanjwa wa kundi lililobaki ndio walipata taatizo hilo.

"Hii ni karibu sawa kwa vikundi vyote viwili “amesema Dkt. Annelies Wilder-Smith, Mshauri wa masuala ya kiufundi wa SAGE na kuongeza kuwa "Kuna utofauti kidogo, lakini bado sio muhimu kitakwimu,"

Hakuna sababu ya damu kuganda kutokana na chanjo

Dkt. Smith amesema "Kwa chanjo yenyewe, hatujaliona tatizo hilo kwenye majaribio, hakuna sababu ya kufikiria na hakuna sababu ya kibaolojia kama tunavyoelewa sasa, kwamba chanjo inaweza kusababisha damu kuganda. Llakini, lazima tuwe wazi kwa matukio mapya yatakayojitokeza, na tunapaswa kuyachukulia kwa uzito. "

Pia ameelezea kuwa wale waliochukuliwa kwa ajili ya chanjo ya majaribiowalichjaguliwa kwa makusudi kwa sababu ni watu ambao walikuwa katika hatari kubwa ya kupata tatizo la kuganda kwa damu.

"Ugonjwa COVID-19  kweli hupeleka wagonjwa katika hali isiyoweza kuambukizwa ya kugandfa kwa damu na kweli vifo vingi ambavyo tunaviona katika wagonjwa walio mahututi wa COVID-19 vinatokana na kuganda kwa damu", Dkt. Smith amesema, kabla ya tangazo linalotarajiwa kutolewa na wakala wa tiba wa Ulaya( EMA) juu ya suala hilo kesho Alhamisi.

Maendeleo hayo yanakuja wakati kuna taarifa za kuongezeka kwa visa vipya vya maambukizo ya coronavirus ulimwenguni kwa asilimia 10 katika wiki iliyopita, na kufikia hadi zaidi ya wagonjwa milioni tatu wapya walioripotiwa.

 

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter