Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zaidi ya nchi 100 zimepokea chanjo dhidi ya Covid-19 kupitia COVAX

Mhudumu wa afya akimpatia chanjo mtu mmzima katika mji wa Lima nchini Peru mwishoni mwa mwezi Mechi 2021.
© UNICEF/Jose Vilca
Mhudumu wa afya akimpatia chanjo mtu mmzima katika mji wa Lima nchini Peru mwishoni mwa mwezi Mechi 2021.

Zaidi ya nchi 100 zimepokea chanjo dhidi ya Covid-19 kupitia COVAX

Afya

Zaidi ya nchi 100 zimepokea chanjo dhidi ya Covid-19 kupitiaCOVAX, ambao ni utaratibu wa mshikamano wa kimataifa uliowekwa na Umoja wa Mataifa na washirika wake kuhakikisha usambazaji wa chanjo kwa uharaka, usawa, salama na ubora. 

Taifa la kisiwa cha Saint Lucia, katika Karibea, ndilo Alhamisi hii limekuwa la 100 kupata chanjo dhidi ya Covid-19, taarifa iliyotolewa hii leo na shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO imetanabaisha.   

Siku 42 baada ya kupeleka chanjo zake za kwanza kwa walengwa wake wa kwanza, Ghana, COVAX ambayo inajumuisha Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa,  WHO na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF wamewezesha zaidi ya dozi milioni 38 zilizotumwa kwa nchi 102 ulimwenguni, 61 ambayo ni za kipato cha chini. 

Chanjo zilizosafirishwa ni pamoja na zile zinazozalishwa na Maabara ya AstraZeneca, Pfizer-BioNTech, na Taasisi ya chanjo ya India. Licha ya kupunguzwa kwa akiba ya chanjo mnamo Machi na Aprili, COVAX inasema inaweza kutoa dozi kwa nchi zote ambazo zimeomba kabla ya mwisho wa Juni. 

Kati ya mataifa 102 ambayo tayari yamepokea chanjo dhidi ya Covid-19 kwa mfumo wa COVAX. Dozi milioni 166 za chanjo hasa AstraZeneca zimetolewa kwa nchi za Kiafrika. 

Kufikia sasa, nchi 45 za kiafrika tayari zimepokea chanjo na 43 zimeanza kuchanja. Lakini Afrika inachukua sehemu ndogo tu ya chanjo ulimwenguni. Kulingana na ofisi ya WHO kanda ya afrika, Afrika imepata asilimia 2 tu ya chanjo milioni 690 zinazosambazwa ulimwenguni kote.  

Bara la Afrika lina watu walioambukizwa Covid-19 takribani milioni 4.3, ambapo 114,000 wamefariki dunia. Katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, eneo la Afrika limeshuhudia maambukizi mapya 74,000 kwa wiki. Wakati huo Kenya inakabiliwa na wimbi la tatu na janga hilo linaonyesha kuongezeka katika nchi zingine 14 za Kiafrika, pamoja na Ethiopia, Eritrea, Mali, Rwanda na Tunisia.