Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Muhogo aina ya Mkombozi yawa mkombozi kwa wakulima Kigoma

Nyuso za furaha kutoka kwa wanakikundi cha Ushindi mkoani Kigoma baada ya mavuno bora kufuatia mafunzo ya mbinu bora za kilimo kutoka FAO ambazo walitumia kwenye shamba darasa.
FAO Tanzania
Nyuso za furaha kutoka kwa wanakikundi cha Ushindi mkoani Kigoma baada ya mavuno bora kufuatia mafunzo ya mbinu bora za kilimo kutoka FAO ambazo walitumia kwenye shamba darasa.

Muhogo aina ya Mkombozi yawa mkombozi kwa wakulima Kigoma

Tabianchi na mazingira

Nchini Tanzania harakati za Umoja wa Mataifa kujengea uwezo wakulima katika kutambua mbinu bora za kilimo kinachohimili mabadiliko ya tabianchi, zimezaa matunda huko mkoani Kigoma baada ya wakulima wa wilayani Kakonko kuvuna zao la muhogo walilopanda kwa kuzingatia ushauri wa wataalamu
 

Katika kata ya Katanga wilayani Kakonko mkoani Kigoma, wakulima wakivuna zao la muhogo kutoka katika shamba darasa walilopatiwa mafunzo na shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO nchini Tanzania kupitia mradi wa pamoja wa Kigoma, KJP. Mkulima huyu akajitambulisha.

Anasema “naitwa Annet John mwanakikundi wa kikundi cha Ushindi, Katanga, nimeushika muhogo wa aina ya Mkombozi ambao tuliupanda baada ya kupata mafunzo Kakonko kutoka kwa mwezeshaji wa FAO. Kwa hiyo sisi kama wanakikundi tumepata faida nzuri sana, tumepata faida ya mafunzo na pia  tumeona ubora wa muhogo unaowahi kukomaa kwa sababu huku kwetu aina hii ya muhogo unaowahi kukomaa haikuwepo. Kwa hiyo tunashukuru sana FAO kwa kutuletea mafunzo na aina hii ya muhogo.”

Mbegu iliyotumika hapa ni Mkombozi, inayohimili siyo tu magonjwa bali pia ukame, na huchukua miezi 10 kukomaa na kuwa tayari kuvunwa. Nashoni Budile ni mkulima mwezeshaji aliyepatiwa mafunzo.

Mkombozi ni kiboko ya batobato

Bwana Nashoni anasema, “na sasa tumefurahi kwa mbegu hii kwa sababu kwanza ilikuwa haijawahi kufika huku na ni mbegu inayokomaa mapema. Lakini jambo lingine sisi kama wakulima wawezeshaji, baada ya kupata mafunzo tuliwafundisha wenzetu namna ya kupanda mihogo ambapo kati ya mche na mche ni mita moja. "

Kuhusu magonjwa amesema "mbegu hii haiumwi sana, kama ile ya kienyeji ambayo haivumilii batobato na majani yananyauka na ukichimba unakuta mizizi tu. Mimi nashauri tutumie mbegu ya Mkombozi kwa sababu inavumilia batobato na unapoenda kuvuna baada ya mwaka mmoja inatoa mihogo mingi.”

Bwana shamba wa kata ya Katanga Masumbuko Masolwa akafunguka kuhusu mbegu Mkombozi akisema, “mbegu hii ya mkombozi ni mbegu ambayo inavumilia mashambulizi ya ugonjwa wa batobato, cha pili, kiwango cha mavuno kwa eneo ni kikubwa kulinganisha na mbegu za kienyeji, cha tatu inawahi kukomaa ukilinganisha na mbegu za kienyeji kwa sababu mkombozi inachukua miezi 9 hadi 12 inakuwa tayari kuvunwa. Mbegu hii kama tulivyosema inavumilia sana magonjwa ambayo ndio kiini cha mavuno madogo katika eneo letu hili.”

Programu ya pamoja kwa mkoa wa Kigoma ilianza mwaka 2017 na mashirika ya Umoja wa Mataifa yanayohusika katika kuongeza mnyororo wa thamani wa zao la muhogo ni pamoja na lile chakula na kilimo, FAO, mpango wa chakula, WFP, kituo cha biashara cha kimataifa, ITC na lile la maendeleo ya mitaji, UNCDF.