Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Yai lililouzwa kwa bei ya hasara sasa lageuka faida, shukrani mashine kutoka FAO

Essau Musinzi, mnufaika wa mashine ya kutotolesha vifaranga vya kuku, mashine ambayo walipatiwa na FAO Tanzania.
FAO Tanzania
Essau Musinzi, mnufaika wa mashine ya kutotolesha vifaranga vya kuku, mashine ambayo walipatiwa na FAO Tanzania.

Yai lililouzwa kwa bei ya hasara sasa lageuka faida, shukrani mashine kutoka FAO

Ukuaji wa Kiuchumi

Baada ya kuhangaika kwa muda mrefu wakipoteza mayai na mara nyingine kuuza mayai kwa bei ya chini kutokana na kukosa uhakika wa kutotolesha mayai kwa kutumia vifaa vya kisasa, hatimaye wafugaji kuku wilayani Kibondo mkoani Kigoma nchini Tanzania sasa wameanza kuona nuru, shukrani kwa kitotoleshi vifaranga au Incubator kwa kiingereza kutoka shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo, FAO. 

Mmoja wa wanufaika wa mashne hiyo Essau Masunzu ambaye ni mwanakikundi toka kikundi cha Jipe Moyo kilichopo eneo la Twabagondozi Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma.

“Kwanza tulipewa mafunzo ya ufugaji bora wa kuku na baada ya hapo tukaomba tupatiwe mashine ya kutotolea vifaranga. Mashine ilifika na tukapewa tena mafunzo ya kuiendesha mashine na kwas asa tumeweza kutotoa vifaranga kwa awamu tatu na awamu ya nne ipo ndani ya Mashine,” amefafanua Bwana Masunzu.

Kando mwa nyumba yenye kitotoleshi ni Paulina Ezron, yeye si mwanakikundi bali ni mnufaika na anasema, “hapa nimekuja kuchukua vifaranga ambavyo nilileta mayai 10 kutoka katika banda langu na nimeweza kupata vifaranga 8. Nimepata huduma ya kutotoleshewa mayai kupitia kikundi cha Jipe Moyo ambao wapo jirani na ninapoishi.”

Mashine ya kutotolesha vifaranga inayomilikiwa na kikundi cha wafugaji kuku cha Jipe Moyo mkoani Kigoma nchini Tanzaina. Walipatiwa mashine hii na FAO Tanzania.
FAO Tanzania
Mashine ya kutotolesha vifaranga inayomilikiwa na kikundi cha wafugaji kuku cha Jipe Moyo mkoani Kigoma nchini Tanzaina. Walipatiwa mashine hii na FAO Tanzania.

Kwa mujibu wa Bwana Masunzu, wanatotoa vifaranga toka kwenye mayai yanayozalishwa na kuku wa kikundi lakini pia wanatoa huduma ya kutotolesha mayai yanayoletwa na jamii kwa bei ya shilingi 500 sawa na senti 25 za dola kwa kila yai moja.

Anasema wamepata manufaa makubwa kwa vile kabla ya kupatiwa mashine “tulikuwa tunauza yai moja kwa senti 25 za dola lakini kwa sasa yai hilo tunalibadili na kuwa kifaranga ambapo tunauza kwa takribani dola moja kwa kifaranga kimoja."

Bwana Musinzi amesema faida nyingine, “ni pamoja na mayai, nyama, fedha kwa matumizi mbalimbali ya nyumbani baada ya mauzo, na pia mbolea ambayo tunaitumia kwenye mashamba yetu.”

Programu ya pamoja kwa mkoa wa Kigoma ilianza mwaka 2017 na mashirika ya Umoja wa Mataifa yanayohusika ni pamoja na lile chakula na kilimo, FAO, mpango wa chakula, WFP, kituo cha biashara cha kimataifa, ITC na lile la maendeleo ya mitaji, UNCDF.