Skip to main content

Watu 670,000 wamelazimika kufungasha virago hadi sasa Cabo Delgado

Wakimbizi wa ndani jimboni Cabo Delgado wakisubiri msaada wa chakula kutoka shirika la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa, WFP kwenye wilaya ya Metuge jimboni Cabo Delgado.
WFP/Falume Bachir
Wakimbizi wa ndani jimboni Cabo Delgado wakisubiri msaada wa chakula kutoka shirika la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa, WFP kwenye wilaya ya Metuge jimboni Cabo Delgado.

Watu 670,000 wamelazimika kufungasha virago hadi sasa Cabo Delgado

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limesema machafuko yanayoendelea kwenye jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbiji hadi sasa yamewalazimisha watu 670, 000 kushafungasha virago na kugeuka kuwa wakimbizi wa ndani huku dunia ikishindwa kuupa kipaumbele mgogoro huo.

Katika makazi ya wakimbizi ya Nanjua B jimboni Cabo Delgado wahudumu wa misaada wa UNHCR wakizungumza na wakimbizi wa ndani kuhusu changamoto zao ambao asilimia kubwa ni wanawake na watoto.

wakimbizi hawa walilazimika kuacha kila kitu ili kuokoa maisha yao. Pamoja na kuwa asilimia kubwa ni wanawake na watoto lakini kuna wanaume pia kama Herculano ambaye familia yake akiwemo mkewe, watoto 10 na wajukuu 8 walilitoroka usiku wa manane katika Kijiji cha Quissanga jimboni humo baada ya nyumba nyingi kijijini kwao kushambuliwa na kuteketezwa kwa moto.  

“Nilikimbia kwa sasbabu ya vita vinavyotuathiri, ulikuwa usiku wa manane hivyo tulikimbia na tukajificha porini. Tulikaa huko msituni kwa siku nne tukitafuta njia ya kutokea  ili kukimbia vita hivyo vilivyoshika kasi.” 

Tangu mwezi Oktoba mwaka jana serikali ya Msumbiji imewahamisha wakimbizi hao wa ndani na kuwaweka katika makazi maalum yaliyoko katika wilaya 9 za jimbo la Cabo Delgado. 

Zaidi ya watu 2,000  wameuawa tangu kuanza kwa mashambulizi mwaka 2017 yakiambatana na unyanyasaji na ukiuwaji mkubwa wa sheria za kimataifa na haki za binadamu. 

Mbali ya vifo machafuko pia yamesambaratisha kabisa maisha ya watu kama Herculano “Maisha yangu Quissanga, nilikuwa nafanyakazi shambani kuzalisha kwa ajili ya kulisha familia yangu na hakukuwa na shida yoyote. Pia nilifanyakazi kama fundi seremala , nilikuwa na karakana yangu na nilikuwa mkulima mfugaji pia. Nilikuwa na mbuzi, kuku, bata na njiwa nyymbani kwangu. Hivyo naona tofauti ya maisha niliyokuwa nayo kule ukilinganisha na haya ya sasa. Ni vigumu sana kwangu kwani tangu nimekuwa hapa sijaweza kupata hata senti.” 

UNHCR inashirikiana na mamlaka kufuatilia na kukidhi mahitaji ya wakimbizi hawa wa ndani na jamii zinazowahifadhi. 

Mgogoro wa Cabo Delgado umezidishwa na kuendelea kwa mashambulizi na janga la corona au COVID-19. Gillian Triggs ni kamishina msaidizi wa UNHCR kwa ajili ya ulinzi.“Hili ni janga kweli la kibinadamu. Janga ambalo linaleta aina mbalimbali za mahitaji ya ulinzi kwa wanawake hawa , wanaume na watoto. Wamekimbia mzozo mbaya kabisa na wamefunga safari za hatari , wengine kwa kutumia mashua, na wengine kupitia nchi kavu ili kupata usalama. 

Pamoja na jitihada za serikali na wadau wa misaada UNHCR inasema rasilimali fedha zinahitajika haraka ili kwenda sanjari na mahitaji ya wakimbizi wa ndani wanaoendelea kumiminika.