Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vurugu mpya kaskazini mwa Msumbiji zimewalazimisha maelfu kuyahama makazi yao

Vurugu zinatokea katika maeneo ambayo tayari yalikuwa na matatizo mengine kama Cabo Delgado ambako tayari kulikuwa kumekumbwa na matatizo ya mafuriko na umaskini
UN Mozambique
Vurugu zinatokea katika maeneo ambayo tayari yalikuwa na matatizo mengine kama Cabo Delgado ambako tayari kulikuwa kumekumbwa na matatizo ya mafuriko na umaskini

Vurugu mpya kaskazini mwa Msumbiji zimewalazimisha maelfu kuyahama makazi yao

Amani na Usalama

Vurugu mpya zinazotokea katika jimbo la Cabo Delgado, kaskazini mwa Msumbiji zimewalazimisha maelfu ya watu kuyakimbia makazi yao, taarifa iliyotolewa hii leo na msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, mjini Geneva Uswisi, imeeleza. 

Bwana Andrej Mahecic amesema kwa ujumla, takribani mashambulizi 28 yametekelezwa katika jimbo hilo tangu kuanza kwa mwaka huu na mashambulizi hayo yanasambaa katika wilaya 9 kati ya 16 za jimbo la Cabo Delgado linalotajwa kuwa moja ya maeneo maskini katika nchi hiyo.

Taarifa hiyo ya UNHCR imesema mashambulizi hivi sasa yanasambaa kuelekea katika wilaya za kusini za Cabo Delgado na kuwalazimisha watu kuhama kuelekea makao makuu ya jimbo hilo katika mji wa Pemba. Tukio la hivi karibuni limetokea kilomita 100 kutoka Pemba.

Andrej Mahecic anasema, "makundi yenye silaha yamekuwa yakiwalenga wanavijiji na kuwatisha watu. Wale ambao wanayakimbia makazi yao wamesimulia kuhusu mauaji, kuumizwa, kuteswa, kucteketezwa kwa nyumba, kuharibiwa kwa mazao na maduka. Tuna taarifa za watu kukatwa vichwa, kutekwa na kupotea kwa wanawake na watoto.”

Ameongeza kuwa wakati mwingine washambuliaji waliwatahadharisha watu kuhusu wapi na wakati gani watashambulia na hivyo ikaleta hofu na kuwafanya watu kuvikimbia vijiji vyao wengi wao wakiacha kila kitu nyuma yao kutokana na kutokuwepo kwa muda wa kubeba mali zao, chakula au hata nyaraka za utambulisho wao.

Akifafanua zaidi kuhusu ukubwa wa tatizo, Bwana Mahecic amesema,“raia wamekimbilia katika maeneo tofautitofauti vikiwemo visiwa vidogo ambako hawana pakuishi. Wengine, wengi wao wakiwa watoto na wanawake wanalala katika hali mbaya na hawana maji safi na salama ya kunywa. Wengi wa wakimbizi wa ndani, IDPs wamekimbilia katika familia au marafiki zao na kuongeza mzigo kwa watu ambao tayari walikuwa katika hali mbaya.”

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, linaongeza msaada kwa watu ambao mahitaji yao yanazidi kuongezeka nchini humo Msumbiji.

Aidha shirika hilo limetoa ombi kwa jumuiya ya kimataifa ili kuongezewa nguvu kwani hivi sasa linalazimika kutenga dola milioni mbili kutoka kwenye miradi yake mingine ili kuwapa watu huduma za awali.