Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi kutoka Cabo Delgado wana kiwewe kufuatia walichoshuhudia- UNHCR

Abdul Selemane ambaye nyumba yake iliteketezwa alikimbia na mama yake, mkewe na wanae kutoka wilaya ya Mocímboa da Praia
FAO/Telcinia Nhantumbo
Abdul Selemane ambaye nyumba yake iliteketezwa alikimbia na mama yake, mkewe na wanae kutoka wilaya ya Mocímboa da Praia

Wakimbizi kutoka Cabo Delgado wana kiwewe kufuatia walichoshuhudia- UNHCR

Wahamiaji na Wakimbizi

Raia waliokimbia mji Palma jimboni Cabo Delgado nchini Msumbiji na kusaka hifadhi maeneo mengine ya nchi ikiwemo mji wa Pemba wamepatiwa angalau misaada kutoka shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR.

Katika uwanja wa michezo wa Pemba, mji mkuu wa jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbiji wakimbizi wamesaka hifadhi baada ya kukimbia mashambulizi ya tarehe 24 mwezi uliopita kutoka kwa watu waliojihami mjini Palma. 

 Hawa ni miongoni mwa watu elfu 11 waliokimbia Palma kwa kutembea au kwa boti , huku wengine wakiripotiwa bado wamenasa kwenye mji huo na wengine wamekwenda miji ya Nangande, Mueda na Montepuez. 

Katika eneo hili wanapatiwa misaada ya matandiko kwa ajili ya malazi, sambamba na nguo, wakionekana wengine wakikagua iwapo zitawafaa au la. 

Margarida Loureiro ni Mkuu wa ofisi ya UNHCR mjini Pemba akisema kuwa katika uwanja huo kuna wakimbizi 270 ambao wanaishi katika mazingira ambayo si ya kiutu lakini angalau wako salama kwa kuwa wana pahala pa kujihifadhi. “Hawa ni watu ambao wamechoka. Wamefika hapa kwa njia mbalimbali, ikiwemo boti siku chache zilizopita na wengine wamewasili hapa kwa kutembea. Hisia hapa ni mchanganyiko kwa kila mtu ambaye nimezungumza naye. Wana kiwewe kwa kile ambacho wameshuhudia kupitia familia au rafiki zao wakiuawa au nyumba zao kuharibiwa kabisa.” 

Miaka mitatu ya mashambulizi kaskazini mwa Msumbiji imesababisha watu takribani Laki 7 kuwa wakimbizi ndani ya nchi yao, wengi wao zaidi mwaka uliopita. 

UNHCR imeonya kuwa idadi hii inaweza kuvuka milioni Moja ifikapo mwezi Juni mwaka huu iwapo ghasia hazitakoma. 

Kwa sasa UNHCR inachukua hatua kupokea wakimbizi zaidi siku zijazo na wafanyakazi wanafika hata maeneo ya nje ya mji wa Pemba ili kusaidia wakimbizi wapya. 

Idadi kubwa ya waliowasili Pemba ni wanawake na watoto wakiwa na virago vichache, watoto wengine wakiwasili bila mzazi au mlezi.