Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Walipiga watu risasi na kuwakata vichwa- Simulizi ya machungu kutoka Cabo Delgado 

Mzozo jimbo la Cabo Delgado kaskazini mwa Msumbiji limepelekea janga la kibinadamu
© WFP/Grant Lee Neuenburg
Mzozo jimbo la Cabo Delgado kaskazini mwa Msumbiji limepelekea janga la kibinadamu

Walipiga watu risasi na kuwakata vichwa- Simulizi ya machungu kutoka Cabo Delgado 

Wahamiaji na Wakimbizi

Jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbiji limekumbwa na ghasia tangu mwaka 2017. Eneo hilo lipo mpakani mwa Tanzania na limeshuhudia ghasia hizo zikifurusha wengine kuvuka mpaka  kuingia Tanzania na wengine kukimbilia maeneo mengine kusaka hifadhi ndani ya nchi yao. Umoja wa Mataifa kupitia mashirika yake likiwemo lile la mpango wa chakula, unahaha kukidhi mahitaji ya kibinadamu. Lakini hali iko vipi kwa wananchi hao? Na Umoja wa Mataifa unataka nini kifanyike zaidi?

Tuko Pemba, mji wa pwani uliko jimboni Cabo Delgado, kaskazini mwa Msumbiji. Eneo lililogubikwa na machafuko, ambako watu waliojihami wanavamia vijiji na kusababisha maelfu ya watu kukimbilia hapa Pemba kusaka hifadhi.  

Wanawake kwa wanaume, vijana na watoto, wanawasili wakiwa na virago vyao wakati huu ambapo mashirika ya Umoja wa Mataifa yanasema bila fedha za kutosha za dharura, basi janga hili la ukimbizi nchini Msumbiji liko hataraini kugeuka janga la njaa kwa kuwa familia zinazidi kukimbia makazi yao huko Palma.  

Ingawa kaweza kujikoa na kufika hapa Pemba, kijana huyu mvuvi Momade Abudala bado shida inamfuata. Amepokea simu kutoka kwa wanafamilia wengine aliowaacha huko Palma, wakiomba fedha ili waweze kukimbia.  

Momade ndio kwanza amewasili kwa boti kutoka Palma na amefika Pemba akiwa na virago vichache ambavyo angalau anaweza kuuza na kisha kupata fedha za kutumia familia yake nyumbani ili hatimaye iungane naye.  

Wakati Momade anawaza na kuwazua, wakimbizi wa ndani ambao tayari wamefika Pemba wamepelekwa katika kambi ya Metuge. Video ya shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani, WFP inaonesha taswira ya juu, vibanda vimesheni! Watoto wanacheza bila kujua kesho yao!   

Lakini mama ni mama ! Viaze Nassir ni mama huyu ! anahakikisha jiko lina moto!   

Anachanja kuni na kisha ni mapishi!! Mboga ikiiva na usafi wa nguo unaendelea!! Kisha akasimulia huku amembeba mwanae!  

“Walianza kupiga risasi na kushambulia kijiji. Wakati huo mwanangu huyu alikuwa amelala ndani ya nyumba. Nilikimbilia ndani kumchukua mtoto, na wao wakaingia. Nilipomchukua, wakapiga kelele..’Wewe wacha! Tutakuua. Mwache, tutakuua! Niliwasihi sana, tafadhali msituue. Nilishaanza kumbeba mtoto. Nilikuwa sina nguo mwilini, sikuwa nimevaa chochote.”  

Janga la Cabo Delgado linaathari kwa watoto na wanawake.
© UNICEF Moçambique/2021/Ricardo Franco
Janga la Cabo Delgado linaathari kwa watoto na wanawake.

Jimbo la Cabo Delgado ni tajri wa mafuta na gesi na tangu mwaka 2017 limekuwa linashuhudia mashambulizi kutoka kwa vikundi visivyo vya kiserikali. Mapigano yameshamiri mwaka mmoja uliopita na watu wamefurushwa mara saba zaidi mwaka huu kuliko mwaka jana.  

Sasa Viaze kwa kuwa hana njia nyingine ya kusaidia watoto wake,  ana ombi moja tu!!  

 “Ningependa watoto wangu wakue na wasome ili wanisaidie na wasaidiane wenyewe kwa sababu sina  njia nyingine. Kwetu tunalima na kuuza mazao kulipia watoto masomo yao. Hapa hilo haliwezekani, tunaishi tu. Hawa ni wanangu na hawana ndugu wengine kwa hiyo wananitegemea mimi tu. Naumia sana nikitambua kuwa wanangu hawa walikuwa na ndugu wa kuwasaidia lakini sasa hawana tena msaada.”  

Watoto wa Viaze na wengine waliosalia na kujikuta kwenye kambi hii ya Metuge wamepitia mengi na wanaonekana wako na nyuso za majonzi na fikra nyingi.  

Watoto wanapimwa iwapo wana utapiamlo au la na kaya zinapatiwa msaada wa chakula kutoka WFP kwa kuwa ndio ngao yao. Msaada huo ni pamoja na mchele na mafuta.   

Punde Viaze baada ya kupata mgao wake anapokea mgeni naye si mwingine bali ni Mkurugenzi Mkuu wa WFP David Beasley. Wameketi na mazungumzo ni kupitia mkalimani.  Anasema wamechoma nyumba na wamekata watu shingo. 

Beasley baada ya mazungumzo akafunguka!  “Hili lilikuwa ni eneo la utalii, uvuvi, uchumi ulikuwa mzuri, watu walikuwa na maisha mazuri lakini sasa? Waasi, magaidi wanatenganisha familia, wanachoma nyumba moto, wanaua watu, wanabaka wanawake ili kuharibu maisha ya watu. Ndio maana WFP sasa tuko hapa tunajaribu kurejesha matumaini kwa watu 715,000 ambao tunawasaidia.”  

WFP inaomba dola milioni 121 zitakazotumika hadi mwisho wa mwaka huu wa 2021 kusaidia wakazi hao zaidi ya Laki Saba wanaoishi katika wilaya za kaskazini za Cabo Delgado akiwemo Viaze.