Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nilichoshuhudia Sudan ni ushahidi wa uwepo wa UNFPA- Dkt. Kanem 

Mkurugenzi mtendaji wa UNFPA wakati alitembelea mama na mtoto hospitalini kwenye wadi jimbo la Blue Nile, Sudan.
Sufian Abdul-Mouty/UNFPA Sudan
Mkurugenzi mtendaji wa UNFPA wakati alitembelea mama na mtoto hospitalini kwenye wadi jimbo la Blue Nile, Sudan.

Nilichoshuhudia Sudan ni ushahidi wa uwepo wa UNFPA- Dkt. Kanem 

Afya

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Idadi ya watu la Umoja wa Mataifa, UNFPA, Dkt. Natalia Kanem amekamilisha ziara yake ya siku tano nchini Sudan ambako pamoja na kupongeza serikali ya mpito na wananchi wake kwa maendeleo yaliyofikiwa nchini humo, ameshuhudia jinsi uwekezaji kwa wanawake na vijana kumekuwa msaada mkubwa hasa katika sekta ya afya ya uzazi.  

Mathalani Umoja wa Mataifa unasaidia serikali katika kuboresha sheria na mifumo halikadhalika haki, usalama na utu wa wanawake na wasichana sambamba na kuweka fursa sawa kwa wote. 

Akiwa ziarani jimboni Blue Nile ambako wanawake wako hatarini kufariki dunia kutokana na uzazi au kujifungua,  Dkt, Kanem ameshuhudia wanawake na vijana wakishiriki katika kuhakikisha afya ya uzazi inakuwa bora halikadhalika masuala ya wajawazito na uzazi salama. 

Dkt. Kanem alikutana na mkimbizi wa ndani Aziza anayeishi kwenye hema. “Aziza ni mwanamke wa kijijini aliyeelimika, aliyekimbia makazi yake ya awali na sasa anaishi Shanisha. Ndoto ya Aziza na kile apendacho zaidi kufanya ni kuwa mwalimu wa shule ya chekechea.” 

Dkt. Kanem anasema alikutana pia na wanawake wengine wa kijijini wenye uwezo mkubwa. 

Akionekana akiwa na wanawake hao, Dkt. Kanem anasema kile kilichomgusa zaidi ni vile ambavyo wamejipanga kwenye usimamizi wa fedha, kwa lengo la kuweza kupatia usafiri wajawazito. 

Anasema katika eneo hilo, mwanamke yoyote aliye hatarini kupoteza maisha wakati wa kujifungua anapatiwa fedha ili aweze kwenda kliniki ya kijamii na hospitali niliyotembelea ilikuwa mfano mzuri wa jins UNFPA inaokoa maisha, hata wakati ambapo huduma ya upasuaji kwenye uzazi inahitajika chini ya mazingira magumu. 

Hata hivyo Mkurugenzi Mtendaji huyu wa UNFPA anasema sehemu bora zaidi ya ziara yake ni pale alipokabidhi funguo ya baiskeli ya magurudumu matatu ambayo hutumika kama gari la wagonjwa. 

“Baiskeli hii inaitwa Tuk Tuk hapa Sudan na kukabidhi funguo kwa mwanamke thabiti kwenye jamii hii, lilikuwa jambo la kufuruhisha zaidi.” 

Na zaidi ya yote ni kuona machifu, watoto, wakunga na wafanyakazi wote wa UNFPA wakiwa pamoja kuhakikisha tunafanikisha lengo la afya. Na hii ndio sababu ya kufanya hivi na ilikuwa siku nzuri.. 

Mkurugenzi Mtendaji huyo wa UNFPA ameshukuru serikali ya Sudan kwa ukarimu wake kwa wakimbizi kutoka nchi jirani. 

Wakati wa ziara hiyo alikuwa na mazungumzo na Waziri Mkuu Abdulla Hamdock, Waziri wa mambo ya nje na kijamii pamoja na viongozi wa ofisi ya Umoja wa MAtaifa nchini Sudan, vijana na viongozi wa kijamii.