Takribani nusu ya wanawake wote katika nchi zinazoendelea, wananyimwa uhuru wao wa mwili: Ripoti ya UNFPA
Takribani nusu ya wanawake wote katika nchi zinazoendelea, wananyimwa uhuru wao wa mwili: Ripoti ya UNFPA
Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu, UNFPA iliyotolewa leo Aprili 14, 2021, takribani nusu ya wanawake wote katika nchi 57 zinazoendelea wananyimwa haki ya kuamua kuhusu miili yao kama vile tendo la ndoa, uzazi wa mpango au kutafuta huduma za afya.
Ripoti ya Hali ya Idadi ya Watu Duniani ni chapisho kuu la UNFPA la kila mwaka na ni ripoti ambayo imekuwa ikichapishwa kila mwaka tangu mwaka 1978, ikiangazia masuala yanayoibuka katika uga wa afya ya kijinsia na uzazi na haki, ikiyaleta masuala haya katika uwazi na pia kuchunguza changamoto zinazoletwa na masuala haya dhidi ya maendeleo ya kimataifa.
Hii ni kwa mara ya kwanza, ripoti ya Umoja wa Mataifa imejikita katika uhuru wa mwili: nguvu na umuhimu wa kufanya uamuzi kuhusu mwili wako bila kuogopa ukatili au mtu mwingine kuamua kwa ajili yako. Mambo yaliyoangaziwa ni pamoja na kulazimishwa kufunga kizazi, kupimwa bikira, ukeketaji na mengine kama hayo.
UNFPA inaeleza kuwa ukosefu huu wa uhuru wa mwili una athari kubwa zaidi ya madhara makubwa kwa wanawake na wasichana kwani inaenda mbali zaidi kuvuruga uzalishaji wa uchumi, kupunguza ujuzi, na kusababisha gharama za ziada kwa huduma za afya nas mifumo ya kimahakama.
Matokeo muhimu: mwili wangu, lakini sio chaguo langu
Kupitia ripoti hii ya msingi, UNFPA inapima nguvu za wanawake kufanya maamuzi yao wenyewe kuhusu miili yao na kiwango ambacho sheria za nchi zinaunga mkono au zinaingilia haki ya mwanamke kufanya maamuzi haya. Takwimu zinaonyesha uhusiano mkubwa kati ya nguvu ya kufanya maamuzi na viwango vya juu vya elimu.
Ripoti hiyo inaonesha kuwa katika nchi ambazo taarifa zinapatikana:
Asilimia 55 pekee ya wanawake wamepewa uwezo kamili wa kufanya uchaguzi juu ya huduma za afya, uzazi wa mpango na uwezo wa kusema ndiyo au hapana kwenye tendo la ndoa.
Ni asilimia 71 tu ya nchi zinahakikisha upatikanaji wa huduma ya uzazi kwa kwa ujumla.
Ni asilimia 75 tu ya nchi ambazo kisheria zinahakikisha upatikanaji kamili, ulio sawa wa uzazi wa mpango.
Ni takribani asilimia 80 pekee ya nchi zina sheria zinazounga mkono afya ya kijinsia na ustawi.
Ni asilimia 56 tu ya nchi zilizo na sheria na sera zinazounga mkono elimu kamili ya jinsia. Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA Dkt Natalia Kanem anasema, "ukweli kwamba karibu nusu ya wanawake bado hawawezi kufanya maamuzi yao kuhusu ikiwa watafanya tendo la ndoa au la, kutumia uzazi wa mpango au kutafuta huduma ya afya inapaswa kutukasirisha sisi sote. Kimsingi, mamia ya mamilioni ya wanawake na wasichana hawamiliki miili yao wenyewe. Maisha yao yanatawaliwa na wengine.”
Ripoti hiyo pia imebainisha njia nyingine nyingi ambazo uhuru wa mwili wa wanawake, wanaume, wasichana na wavulana unakiukwa, ikiweka wazi kwamba:
Nchi ishirini zina sheria za "kuolewa na aliyekubaka", ambapo mwanamume anaweza kuyakwepa mashtaka ya jinai ikiwa atamuoa mwanamke au msichana aliyembaka.
Nchi arobaini na tatu hazina sheria inayoshughulikia suala la ubakaji wa ndani ya ndoa, yaani pale ambapo mtu anabakwa na mwenzi wake ndani ya ndoa.
Zaidi ya nchi 30 zinazuia haki ya wanawake hata kutembeatembea nje ya nyumba zao. Na kwamba wasichana na wavulana wenye ulemavu wako karibu mara tatu zaidi ya kufanyiwa unyanyasaji wa kijinsia, wasichana wakiwa katika hatari kubwa zaidi.
Suluhisho: nguvu ya kusema ndio, haki ya kusema hapana
Ripoti inaonesha jinsi juhudi za kushughulikia unyanyasaji zinaweza kusababisha ukiukaji zaidi wa uhuru wa mwili. Kwa mfano, katika kuhukumu kesi ya ubakaji, mfumo wa haki ya jinai unaweza kuhitaji manusura kufanyiwa upimaji wa kile kinachoitwa upimaji wa ubikira.
Ripoti inasema suluhisho halisi lazima lizingatie mahitaji na uzoefu wa wale walioathiriwa. Kwa mfano, nchini Mongolia, watu wenye ulemavu wamewekewa mpango wa kutoa maoni moja kwa moja kwa serikali juu ya mahitaji yao ya afya ya uzazi na uzazi. Nchini Angola, vijana walioelimishwa kuhusu miili yao, afya na haki wameweza kutafuta huduma za afya, kutumia uzazi wa mpango kupungua ngono na kuomba haki baada ya unyanyasaji wa kijinsia.
"Kunyimwa uhuru wa mwili ni ukiukaji wa haki za kimsingi za wanawake na wasichana ambazo zinaimarisha usawa na huendeleza unyanyasaji unaotokana na ubaguzi wa kijinsia. Hakuna kitu isipokuwa kuangamiza msukumo, na lazima ikome.” Anasema Dkt Kanem.
Kisha Dkt Kanem anaongeza akisema, "kinyume chake, mwanamke ambaye ana udhibiti juu ya mwili wake ana uwezekano mkubwa wa kuwezeshwa katika nyanja nyingine za maisha yake. Anapata sio tu kwa suala la uhuru, lakini pia kupitia maendeleo katika afya na elimu, mapato na usalama. Ana uwezekano mkubwa wa kufanikiwa, na familia yake pia.”