Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mapambano dhidi ya fistula, yanaweza kuathiriwa na janga la sasa la COVID-19-UN 

Manusura wa Fistula wakipewa huduma ya afya nchni Tanzania
© UNFPA Tanzania/Bright Warren
Manusura wa Fistula wakipewa huduma ya afya nchni Tanzania

Mapambano dhidi ya fistula, yanaweza kuathiriwa na janga la sasa la COVID-19-UN 

Afya

Mapambano ya kutokomeza tatizo la fistula, moja ya majeraha ya hatari yanayotokea wakati wa kujifungua, yanaweza kuhatarishwa na janga la sasa la virusi vya corona au COVID-19, umetahadharisha ujumbe wa Umoja wa Mataifa kuhusu siku ya kimataifa ya kutokomeza fistula inayoadhimishwa kila tarehe 23 ya mwezi Mei kila mwaka. 

Fistula ni ugonjwa ambao husababisha shimo kubwa kati ya njia ya uzazi na njia ya mkojo unatokana na mama kuwa na uchungu wa muda mrefu bila matibabu. Kwa mujibu wa UNFPA mara nyingi ugonjwa huu huwapata wanawake na wasichana masikini kabisa na wanaotoka jamii zilizotengwa. Fistula inayohusishwa na uzazi inaweza kuzuiwa kwa kuchelewesha uzazi wa kwanza, yaani kwa kusubiri umri sahihi, kutokomeza njia za kimila ambazo ni hatarishi na pia kuhakikisha upatikanaji wa huduma za uzazi kwa muda muafaka. 

Ujumbe kutoka Umoja wa Mataifa kuhusu siku hii umeendelea kueleza, “hata hivyo hivi sasa juhudi zote zimeelekezwa katika mapambano dhidi ya virusi vya corona, na matatizo mengine yameachwa bila kushughulikiwa. Kwa bahati mbaya, janga la sasa linavuruga hatua za kuzuia fistula katika nchi zinazoendelea ambako mifumo ya afya, hata kabla ya mlipuko wa virusi vya corona, mar azote haikuwa na uwezo wa kutoa huduma ya tiba ambayo mtu anaweza kuimudu na iliyo na kiwango cha juu kinachohitajika.”

Ujumbe huo umetoa mfano kuwa, inatabiriwa kuwa kufikia mwaka 2030, ndoa za utotoni milioni 13 zinaweza kutokea kutokana na uwepo wa COVID-19 kuliko ambavyo ingekuwa katika hali ya kawaida. Wazazi wanataka kuwaozesha watoto wao mapema iwezekanavyo ili kupunguza uzito wa mzigo walio nao kutokana na hali mbaya ya uchumi.

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na idadi ya watu duniani, UNFP kuhusu siku hii ya kimataifa ya kutokomeza fistula limesema “janga hili la COVID-19 linategemewa pia kuchelewesha utekelezaji wa programu zinazolenga kutokomeza matendo yasiyo ya kibinadamu ya ukeketaji. Kwa mujibu wa UNFPA, ukeketaji ni moja ya visababishi vya kuendelea kwa fistula inayohusishwa na uzazi.” 

Wakati virusi vikizidi kusambaa, huduma za afya zinaweza kutoa huduma chache tu katika zile ambazo wanawake wanazihitaji. Wakati huo huo wanawake wengi na wasichana, kwa kuogopa COVID-19, hawaendi kuwaona madaktari. 

Timu ya madaktari ambao wanatibu fistula katika hospitali ya Al Thawara nchini Yemen
©UNFPA Yemen
Timu ya madaktari ambao wanatibu fistula katika hospitali ya Al Thawara nchini Yemen

 

Ahadi ya kuboresha afya na haki za wanawake na wasichana inajaribiwa kuliko wakati mwingine wowote

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu, UNFPA , Natalia Kanem, kupitia ujumbe wake alioutoa kuhusu siku hii ya kimataifa ya kutokomeza fistula amesema mwezi Novemba mwaka jana 2029 dunia ilikutana mjini Nairobi Kenya kusherehekea mafanikio makubwa ya miaka 25 katika kuendeleza haki na afya ya wanawake na wasichana. Viongozi duniani kote kuanzia marais hadi ngazi ya chini kabisa, wakimbizi, vijana na wakurugenzi, waliweka ahadi ya kusongesha harakati na hatua za kuhakikisha afya ya uzazi na jinsia pamoja na haki kwa wote. Hata hivyo akaongeza, “miezi sita tu baadaye, ahadi hiyo inajaribiwa kuliko wakati mwinginme wowote. Mifumo ya afya inahangaika kupambana na COVID-19, janga ambalo linaweza kuathiri afya ya mama na watoto wachanga.” 

Daktari akizungumza na mmoja wa wagonjwa wa Fistula.
UNFPA/Ollivier Girard
Daktari akizungumza na mmoja wa wagonjwa wa Fistula.

 

Kama kiongozi wa kimataifa wa kampeni ya kutokomeza fistula, UNFPA inatoa ufadhili wa kusaidia kuzuia fistula, pamoja na tiba. Tangu mwaka 2003, shirika hilo la Umoja wa Mataifa limewasaidia wanawake 113,000 kufanyiwa upasuaji wa fistula na kuwarejesha katika hali yao ya kawaida.