Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Askari walinda amani wanawake kutoka Tanzania wawatembelea wanawake Beni, DRC

Walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Tanzania wanaohudumu MONUSCO nchini DRC wakizungumza na wananchi wakazi wa jimbo la Kivu Kaskazini.
TANZBATT_8/Kapteni Tumaini Bagambo.
Walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Tanzania wanaohudumu MONUSCO nchini DRC wakizungumza na wananchi wakazi wa jimbo la Kivu Kaskazini.

Askari walinda amani wanawake kutoka Tanzania wawatembelea wanawake Beni, DRC

Amani na Usalama

Kikundi cha walinda amani wanawake kutoka Tanzania katika kikosi cha nane kinachohudumu katika Ujumbe wa Umoja wa Mataifa FIB MONUSCO, nchini DRC, kimewatembelea wanawake wa kata za Matembo, Nzuma na Ngadi wilaya ya Beni. 

Hii ni ziara yao ya kwanza tangu kuwasili kwa TANZBATT-8 Jimboni Kivu Kaskazini mapema Januari 9, 2021 tayari kwa jukumu la ulinzi wa amani nchini DRC. 

Meja Pracksidia Lwekamwa ni kiongozi wa walinda amani wanawake kutoka Tanzania kundi la 8 akieleza lengo la ziara hiyo amesema, “tumekuja kijiji cha Mavivi ili kuonana na wanawake wa Mavivi kujua changamoto wnazokabiliana nazo. Tumegundua changamoto walizonazo ni nyingi kwa hivyo zile ambazo ziko chini ya uwezo wetu tutazifanyia kazi, na ambazo ziko nje ya uwezo wetu, tutazichukua.”

Habari za UN-Wanawake wa TANZBATT_8 wawatembelea wanawake wa Beni.

 

Pamoja na mambo mengine suala la mahusiano kati ya walinda amani na raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo linapewa kipaumbele, Kapteni  Werema  Getenyi ni Afisa mahusiano kati  ya raia na Jeshi anasema, “tunazunguka maeneo mbalimbali kwa ajili ya kuimarisha mahusiano. Tumeelewa matatizo yao, tutajaribu kuyashughulikia kwa kadri uwezo wetu utakavyokuwa.” 

Kwa upande wao viongozi na raia wa kata hizo wanaeleza namna walivyo pokea ujio wa walinda amani hao. Kasoki Vaitsola Nadine ni mwanamke mkazi wa Matembo anasema anawashukuru sana askari hao wa kike kutoka Tanzania kwa kitendo chao cha kuwatembelea, na kwamba wasiishie hapo, “kwani tunajua mcongomani na mtanzania ni kitu kimoja. Msituchoke, tunasema asante sana.”