Skip to main content

Vijana wajitoa kimasomaso kulinda walio taabuni

Justina Joseph Manengwa ni mlinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Tanzania ambaye sasa yuko kwenye jukumu la ulinzi wa amani kwenye ujumbe wa MONUSCO nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC.
MONUSCO

Amani na Usalama

Kuelekea siku ya walinda amani duniani tarehe 29 mwezi huu wa Mei, tunamulika walinda amani vijana waliojitolea maisha yao ugenini ili kulinda wengine wasio na uwezo wa kujilinda katika nchi zao. Hii ni kwa kuzingatia kuwa ujumbe wa mwaka huu ni Kuelekea amani ya kudumu: Matumizi ya nguvu ya vijana kwa ajili ya amani na usalama.

Ujumbe huu unazingatia kuwa leo hii, makumi ya maelfu ya walinda amani vijana wenye umri wa kati ya miaka 18 hadi 29 wamepelekwa katika operesheni mbalimbali za Umoja wa Mataifa kote duniani kwa lengo kuu la kusaidia kutekeleza majukumu ya ulinzi wa amani na raia. Sasa Umoja wa Mataifa kupitia maazimio ya Baraza la Usalama namba 2250, 2419 na 2535 unaongeza ushirikiano na vijana ili kusaidia kusongesha amani.

Na ni kwa kuzingatia hilo tunaelekea nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC kumulika vijana wa kitanzania wanaohudumu katika kikosi cha 8, TANZBATT-8 kwenye Brigedi ya kujibu mashambulizi, FIB ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, MONUSCO. Kituo chao ni Beni, jimboni Kivu Kaskazini.

Vijana wa Tanzania ndani ya FIB ya MONUSCO

Private  Monica Constantino Nyagawa, analinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC chini ya bendera ya Umoja wa MAtaifa. Yeye anatoka Tanzania.
MONUSCO
Private Monica Constantino Nyagawa, analinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC chini ya bendera ya Umoja wa MAtaifa. Yeye anatoka Tanzania.

Kutana na mlinda amani Private Monica Constantino Nyagawa. Huyu ana umri wa miaka 24 na jukumu lake katika TANZBATT-8 ni afisa muuguzi katika kituo cha afya cha Beni kinachohudumia siyo tu walinda amani bali pia wananchi.

Private Nyagawa anasema kile anachopenda zaidi kuhusu kazi yake ni kutoa huduma kwa walinda amani wenzake na raia ili kuimarisha afya zao na kisha waendelee na majukumu yao.

Lakini kubwa zaidi ni kile alichojifunza kwenya jukumu lake hili nchini DRC akisema, "nimejifunza mambo mengi sana kuhusu kazi yangu, mathalani kudhibiti majeraha na vile vile kuyakinga. Kuwapatia matumaini na ujaziri wagonjwa na kuwafundisha walinda amani wenzangu jinsi ya kuepusha, kujikinga na kudhibiti magonjwa."

Katika eneo lao la Beni, jimboni Kivu Kaskazini Ebola ilikuwepo lakini sasa imedhibitiwa, halikadhalika ugonjwa wa Corona au COVID-19 ambapo walinda amani pia wamejifunza jinsi ya kujikinga na maambukizi kwa kuvaa barakoa.

Stephano Odhimbo, mlinda amani kutoka Tanzania akihudumu chini ya bendera ya Umoja wa Mataifa huko DRC.
MONUSCO
Stephano Odhimbo, mlinda amani kutoka Tanzania akihudumu chini ya bendera ya Umoja wa Mataifa huko DRC.

Mlinda amani mwingine kijana katika TANZBATT-8 ni Stephano Joshua Odhiambo. Yeye ana umri wa miaka 24 na anasema kile anachopenda zaidi kwenye kazi yake ni "kuwa miongoni mwa wale waliochaguliwa kupigana kwa ajili ya watu wanaohitaji amani na maisha ya kawaida hapa DRC. Hii ni kwa sababu siyo kila mmoja anaweza kuingia vitani na kuleta amani kwenye eneo lake. Kitu kingine ni kwamba nashirikiana na askari wenzangu ili kuona watu wanaishi kwa amani, na hii inanifanya niwe na furaha na kuongeza motisha wangu wa kuendelea kufanya kazi kwa bidii."

Alipoulizwa kile ambacho amejifunza tangu kufika DRC mapema mwaka huu, Odhiambo anasema ni amani. "Amani ni muhimu sana. Kama mlinda amani nimeona na kujifunza mno, jinsi ambavyo raia wasio na hatia wanataabika. Kwa hiyo nchi ambazo zina amani lazima ziendelee kuilinda kwa sababu pindi inapotoweka ni vigumu sana kuirejesha."

Justina Joseph Manengwa ni mlinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Tanzania ambaye sasa yuko kwenye jukumu la ulinzi wa amani kwenye ujumbe wa MONUSCO nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC.
MONUSCO
Justina Joseph Manengwa ni mlinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Tanzania ambaye sasa yuko kwenye jukumu la ulinzi wa amani kwenye ujumbe wa MONUSCO nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC.

Mlinda amani mwinigine kijana zaidi TANZBATT-8 ni Justina Joseph Manengwa. Mtanzania huyo mlinda amani nchini DRC anasema "kama mlinda amani mwanamke, mazingira yangu ya kikazi jeshini yameniweka katika maeneo mengi ya kujifunza kama vile kuwa na uwezo wa kuwakilisha wanawake wapiganaji katika wajibu mkubwa wa kulinda raia, wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na vifaa. Vile vile nimeweza kujifunza kuhusu utofauti wa tamaduni baina ya jamii tofauti."

Kuhusu kile alichojifunza tangu kuanza jukumu lake nchini DRC, Justina anasema "amani ni rasilimali ambayo inapaswa kulindwa kwa gharama yoyote. Pale amani inapotoweka, makundi yaliyo hatarini zaidi kama vile wanawake na watoto ndio yanayotaabika."