Skip to main content

UN na ECOWAS walaani machafuko baada ya kutangazwa matokeo ya awali ya uraisi Niger

Mfanyakazi wa UNICEF akisaidia kampeni ya kuhamasisha umma kuhusu COVID-19
© UNICEF/UNI322709/Haro
Mfanyakazi wa UNICEF akisaidia kampeni ya kuhamasisha umma kuhusu COVID-19

UN na ECOWAS walaani machafuko baada ya kutangazwa matokeo ya awali ya uraisi Niger

Amani na Usalama

Umoja wa Mataifa na jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi ECOWAS leo wamelaani machafuko nchini Niger kufuatia tangazo la matokeo ya awali ya duru ya pili ya uchaguzi wa rais tarehe 21 Februari.

Katika tarifa yao ya pamoja, Umoja wa Mataifa na tume ya ECOWAS wamesema wanatambua tanggazo hilo la matokeo ya awali lililotolewa na tume huru ya uchaguzi ya Niger.

Wakikumbushia hitimisho lililofanywa na timu ya uangalizi ya ECOWAS wamewapongeza watu wa Niger kwa uhamasishaji mkubwa na ushiriki wa amani katika uchaguzi huo wa Rais.

“ECOWAS na Umoja wa Mataifa tunalaani vikali vitendo vya machafuko ambavyo vimefanyika kufuatia tangazo la matokeo ya awali ya uchaguzi na tunatoa wito kwa wadau wote kujizuia na machafuko zaidi” imesema tarifa ya pamoja ya vyombo hivyo viwili.

Mashirika hayo mawili yamewataka wadau wote “Kuzingatia mfumo wa sheria ambao unahakikisha mchakato mzima wa uchaguzi unafanyika kwa njia ya amani, hususan ule unaohusiana na kutatua mivutano ya uchaguzi, na kuwachagiza kushirikiana ili kukamilisha mchakato wa uchaguzi.”

Pia mashirika hayo ECOWAS na Umoja wa Mataifa yamerejea kauli yao ya kusaidia watu wa Niger katika juhudi zao za kudumisha amani na demokrasia.

Jumanne wiki hii tume huru ya kitaifa ya uchaguzi nchini Niger ilitangaza ishindi wa asilimia 55.7% ya kura kwa mgombea wa uchaguzi wa chama tawala Mohamed Bazoun dhidi ya yule wa chama cha upinzani Mohamane Ousmane ambaye amepinga matokeo hayo na kudai kwamba yeye ni mshindi kwa kupata asilimia 50.3% ya kura.

Tangu kutangazwa kwa matokeo hayo machafuko yamezuka katika mji mkuu Niamey na katika miji mingine nchini humo, huku watu wakiandamana mitaani na kushambulia vikosi vya usalama ambavyo vimekuwa vikitumia mabomu ya kutoa machozi kudhibiti maandamano hayo.