Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa UN akaribisha kurejea kwenye makubaliano ya uchaguzi nchini Somalia 

Mbunge katika bunge la Somalia, akipiga kura katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais mwaka 2017. Katika mabadiliko ya katiba uchaguzi ujao utakuwa mtu mmoja kura moja.
UN Photo/Ilyas Ahmed)
Mbunge katika bunge la Somalia, akipiga kura katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais mwaka 2017. Katika mabadiliko ya katiba uchaguzi ujao utakuwa mtu mmoja kura moja.

Mkuu wa UN akaribisha kurejea kwenye makubaliano ya uchaguzi nchini Somalia 

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Jumamosi amekaribisha uamuzi wa bunge dogo la baraza la shirikisho nchini Somalia la kubatilisha sheria maalum na kurejea kwenye mkataba wa uchaguzi wa Septemba 17 ambao utaruhusu kufanyika kwa uchaguzi wa rais na wabunge usio wa moja kwa moja. 

Katika taarifa iliyotolewa na msemaji wake, Katibu Mkuu António Guterres amesisitiza wito wake kwa wadau wote wa Somalia "kuanza mazungumzo mara moja na kufikia muafaka juu ya kufanyika kwa uchaguzi ulio jumuishi bila kucheleweshwa zaidi". 

Taarifa hiyo imeongeza kuwa "Katibu Mkuu anasisitiza umuhimu wa makubaliano yenye wigo mapana Zaidi kwa ajili ya utulivu wa nchi". 

Ujumbe wa Usaidizi wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia (UNSOM) pia umekaribisha uamuzi wa baraza la bunge hilo dogo wa kurejesha makubaliano ya uchaguzi. 

Sheria maalum ya uchaguzi wa shirikisho ilipitishwa na baraza la bunge dogo mnamo Aprili, ikiruhusu kuongezewa muda kwa Rais Mohamed Abdullahi Mohamed kwa kipindi cha miaka miwili zaidi  baada ya muda wake kumalizika rasmi mwezi Februari. 

Ongezeko hilo la muda  lilisababisha mapigano kati ya wanaounga mkono Serikali na wafuasi wa upinzani katika mji mkuu wa Mogadishu na pia katika maeneo mengine ya nchi, wakati kukiwa na wasiwasi kwamba kundi lenye msimamo mkali la Al Shabaab linaweza kutumia mgawanyiko huo kwa faida yake, kulingana na ripoti za vyombo vya habari. 

Taartifa za vyombo vya Habari pia zimesema kwamba kuna makumi ya maelfu ya watu waliokimbia makwao wakihofia usalama wao kufuatia vurugu hizo.