Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Makundi yaliyojihami DRC yaua raia na kutoza wananchi kodi za kuingia mashambani- UNHCR

UNHCR inasema mauaji na utekaji nyara vimeendelea jimboni Kivu Kaskazini nchini DRC mwaka huu wa 2021
© UNHCR/Frederic Noy
UNHCR inasema mauaji na utekaji nyara vimeendelea jimboni Kivu Kaskazini nchini DRC mwaka huu wa 2021

Makundi yaliyojihami DRC yaua raia na kutoza wananchi kodi za kuingia mashambani- UNHCR

Wahamiaji na Wakimbizi

Makundi yaliyojihami huko jimboni Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, yameendelea kutekeleza mauaji na vitendo vya kikatili na dhalili kwa wakazi wa enoe hilo hata mwaka huu wa 2021.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limetolea mfano kuwa tarehe 24 mwezi uliopita, watu wenye silaha walivamia eneo la makazi ya wakimbizi wa ndani huko Masisi jimboni Kivu Kaskazini na kuuawa watu wawili na kujeruhi wengine sita.

Msemaji wa UNHCR mjini Geneva, Uswisi Babar Baloch amewaambia waandishi wa habari hii leo kuwa wiki moja kabla ya shambulio hilo, kundi la watu wenye silala liliteka nyara watu wawili kutoka eneo la makazi ya wakimbizi wa ndani huko Kivuye, eneo ambalo linapata usaidizi kutoka UNHCR.

“Kundi hilo pi lilitangaza amri ya watu kutotembea kuanzia saa moja usiku ambapo baada ya kuweka amri hiyo walitembelea kila nyumba kutaka wakazi walipe malipo ya ulinzi,” amesema Bwana Baloch.

Manusuru wa mashambulizi hayo wasimulia masahibu

UNHCR na wadau wake wamepata simulizi kadhaa kutoka kwa manusura wa ghasia za kuanzia Desemba 2020 hadi Januari 2021 ambapo kumekuwepo na matukio kama saba ya watu wenye silaha kuvamia maeneo na kati ya mashambulizi hayo, matano ni katika eneo la Masisi.

Zaidi ya wakimbizi wa ndani 88,000 wanaishi kwenye maeneo 22 yanayopatiwa msaada na UNHCR na shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM ilihali asilimia 90 ya watu hao wanaishi na wenyeji.

UNHCR imepokea ripoti ya kwamba vikundi vilivyojihami vinashikilia shule, nyumba na kuzuia shughuli za shuleni, sambamba na kushambulia vituo vya afya kwenye maeneo ya Masisi na Lubero.

Rutshuru waasi waanzisha ushuru kwa waendao mashambani

Mwezi Novemba mwaka jana vikundi hivyo vilianzisha ushuru usio halali huko eneo la Rutshuru kwa ajili ya watu wanaokwenda kwenye mashamba yao.

“Hatua hiyo ilisababisha watu wengi washindwe kujipatia chakula na mbinu za kujipatia kipato,” amesema Bwana Baloch akiongeza kuwa wakimbizi wa ndani hawana uwezo wa kulipa ushuru huo kwa kuwa hawana kipato.

Tweet URL

Inashukiwa kuwa mashambulizi yanayofanywa na vikundi vilivyojihami hutekelezwa kwa ushirikiano na vikundi vingine au jeshi la serikali ya DRC ambapo raia wanajikuta wako katikati ya mzozo baina ya makundi tofauti.

Wakati operesheni za kijeshi za jeshi la serikali dhidi ya wanamgambo waliojihami zilikuwa na mafanikio makubwa hapo awali, hivi sasa jeshi la serikali halina uwezo wa kudhibiti maeneo mengi, na hivyo kuacha nafasi kubwa kwa waasi kudhibiti maeneo hayo na kuweka masharti yao kwa wananchi.

UNHCR inatoa wito kwa pande zote kuheshimu sheria za kibinadau na kutaka uchunguzi wa haraka wa uhalifu uliotekelezwa ili wahusika wafikishwe mbele ya sheria.

Zaidi ya watu milioni tano wamefurushwa makwao kutokana na ghasia DRC katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, ambapo kati yao hao, milioni mbili wako jimboni Kivu Kaskazini pekee huku UNHCR ikikabiliwa na ukata katika operesheni zake za usaidizi.

Hadi sasa ombi la kusadia operesheni za UNHCR nchini DRC la dola milini 195 limefadhiliwa kwa asilimia sita pekee.