Mapigano Kivu Kaskazini ‘mwiba’ kwa harakati dhidi ya Ebola- UNHCR

24 Agosti 2018

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, mapigano yanayoendelea katika jimbo la Kivu Kaskazini yanatishia harakati za kukabiliana na ugonjwa wa Ebola uliolipuka jimboni humo mwezi uliopita. John Kibego na taarifa kamili.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR linaripoti ghasia kwenye eneo liliitwalo pembetatu ya kifo likijumuisha miji ya

Eringeti, Mbau na Kamango, mpakani mwa Uganda na DRC pamoja na miji ya Beni, Oicha na Mavivi jimboni Kivu Kaskazini.

Wafanyakazi wa UNHCR wameshuhudia vijiji vitupu, nyumba zilizotekelezwa na magari yaliyochomwa moto wakati huu wakihaha kukabili Ebola iliyosababisha vifo vya watu 63 hadi sasa jimboni humo.

Mapigano ni kati ya vikundi  kadhaa vilivyojihami na yameshamiri katika miji yote sita ya jimbo la Kivu Kaskazini, raia wakisimulia ukatili wa kutisha ikiwemo kukatwa mapanga na mauaji. Andrej Mahecic ni msemaji wa  UNHCR, Geneva Uswisi.

(Sauti ya Andrej Mahecic)

“UNHCR ina wasiwasi zaidi kutokana na kuendelea kuzorota kwa hali ya usalama kwenye eneo la Beni ambalo limekumbwa na Ebola. Eneo hili ni makazi ya watu milioni 1.3.”

Bwana Mahecic amesema mahitaji ya kibinadamu yanaongezeka huku hofi ya kuenea kwa Ebola ikitanda kwa hiyo wanaimarisha usaidizi wao ili kukidhi mahitaji ya wakimbizi wa ndani  huko Beni, akisema...

(Sauti ya Andrej Mahecic)

“Wakati UNHCR ikiendelea na usaidizi wa kibinadamu licha ya mlipuko wa Ebola, mdororo wa usalama na ukosefu wa fedha unakwamisha jitihada zetu. Ombi la dola milioni 201 lililotolewa na UNHCR kusaidia DRC mwaka 2018 limefadhiliwa kwa asilimia 17 pekee.”

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud