Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mamia wauawa kwenye ghasia zinazoendelea Mashariki mwa DRC

Odette akiwa amepiga picha na wazazi wake kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani ya Plaine Savo  jimboni Ituri ambako waasi wa CODECO walishambulia na kumkata panga la usoni. Alipotezana na wazazi wake na sasa wamempata.
© UNHCR/Hélène Caux
Odette akiwa amepiga picha na wazazi wake kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani ya Plaine Savo jimboni Ituri ambako waasi wa CODECO walishambulia na kumkata panga la usoni. Alipotezana na wazazi wake na sasa wamempata.

Mamia wauawa kwenye ghasia zinazoendelea Mashariki mwa DRC

Wahamiaji na Wakimbizi

Hali ya usalama inazidi kuwa mbaya huko Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC hususa jimboni Ituri ambako vikundi vilivyojihami vimeendelea kuua rai ana katika wiki sita zilizopita zaidi ya raia 200 wameuawa, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi duniani, UNHCR. 

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi hii leo, msemaji wa UNHCR Eujin Byun amesema hali hiyo intatia wasiwasi zaidi shirika hilo kutokana na kuendelea kwa mashambulio hayo ya kikatili kwani katika kipindi cha wiki sita, pamoja na mauaji ya raia, makundi hayo yaliyojihami yameharibu nyumba 2,000, pamoja na shule 80 huku takribani watu 52,000 wakikimbia makazi yao. 

UNHCR inasema tayari Ituri ina zaidi ya wakimbizi wa ndani milioni 1.5. 

Shambulio la karibuni zaidi ni la tarehe 19 mwezi huu huko kambi ya wakimbizi wa ndani Plaine Savo ambako watu wenye silaha walivamia na kuua watu 7 wakiwemo watoto watano. 

Kati ya wakimbizi hao wa ndani milioni 1.5, elfu 35wamesaka hifadhi kwenye kituo cha wakimbizi wa ndani cha Rhoe ambako miundombinu ya dharura kwa ajili ya makazi, vyoo na majiko ya umma imezidiwa uwezo kwa kuzingatia kituo hicho sasa kinahifadhi watu 70,000 takribani maradufu ya idadi inayotakiwa. 

Mvulana mwenye umri wa miaka 14 akiwa amelazwa hospitalini baada ya familia yake kushambuliwa kwa mapanga na watu wenye silaha kwenye kijiji chao huko Bunia jimboni Ituri nchini DRC. Anayemwangalia ni shangazi yake.
© UNHCR/Hélène Caux
Mvulana mwenye umri wa miaka 14 akiwa amelazwa hospitalini baada ya familia yake kushambuliwa kwa mapanga na watu wenye silaha kwenye kijiji chao huko Bunia jimboni Ituri nchini DRC. Anayemwangalia ni shangazi yake.

Hali si shwari pia Kivu Kaskazini 

Bwana Byun amesema katika jimbo jirani la Kivu Kaskazini nako hali si shwari tangu kuibuka tena kwa mashambulizi mwezi Machi mwaka jana wa 2022 na hadi sasa watu 521,000 wamekimbia makazi yao kutokana na mashambulizi ya kutoka angani, halikadhalika kukwepa kutumikishwa vitani na vikundi vilivyojihami. 

Takribani watu 120,000 wamekimbia ili kusaka usalama kwenye viunga vya mji mkuu wa Kivu Kaskazini, Goma wakiwa na virago vyao kichwani na watoto wao mgongoni. 

Kwa ujumla watu milioni 2.1 wamekimbia makwao jimboni Kivu Kaskazini. 

UNHCR na wadau wanaendelea kutoa misaada ya kuokoa maisha 

Msemaji huyo amefafanua kuwa licha ya ukosefu wa usalama, UNHCR na wadau wanaendelea kupatia misaada ya kuokoa maisha wakimbizi wa ndani. 

Vijiji vingi mjini Djugu jimboni Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC vimetelekezwa kutokana na mashambulizi ya kundi la CODECO.
UNHCR/Hélène Caux
Vijiji vingi mjini Djugu jimboni Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC vimetelekezwa kutokana na mashambulizi ya kundi la CODECO.

“Mwezi januari tumesaidia familia 1,154 za watu wenye ulemavu, wajawazito na wale walio hatarini zaidi kuhamia makazi mapya ya dharura kwenye kituo cha wakimbizi wa ndani cha Buchagara karibu na Goma. Na huko Ituri tunaongeza makazi ya mahema 1,000 kwenye kituo cha Rhoe.” 

UNHCR inasema ujenzi wa Buchagara umeendelea licha ya shirika hilo kupokea asilimia 46 tu ya mahitaji yake kwa mwaka 2022, “lakini hii imewezekana kutokana na kuweka vipaumbele kwenye mahitaji muhimu kam avile elimu. Kwa mwaka 2023 UNHCR inatahijia dola milioni 233 ili kusaidia wakimbizi wa ndani DRC.” 

Nchini DRC zaidi ya watu milioni 5.6 ni wakimbizi wa ndani na hivyo kufanya taifa hilo kuwa nchi inayoongoza barani Afrika kwa kuwa na idadi kubwa walio wakimbizi wa ndani na pia duniani kote. DRC pia ni nyumbani kwa wakimbizi 524,700.