Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tumejipanga ili kutoa mchango bora zaidi katika vikundi vipya vya ulinzi wa amani DRC- Meja Jenerali Kapinga

Walinda amani kutoka Tanzania na Indonesia wakikagua daraja.
TANZBATT 7/Ibrahim Mayambua
Walinda amani kutoka Tanzania na Indonesia wakikagua daraja.

Tumejipanga ili kutoa mchango bora zaidi katika vikundi vipya vya ulinzi wa amani DRC- Meja Jenerali Kapinga

Amani na Usalama

Wakati Tanzania ikijiandaa kupeleka kikosi chake katika vikundi vipya vitakavyokuwa na uwezo wa kuchukua hatua haraka zaidi kukabiliana na vitisho na hatimaye kuimarisha ulinzi wa raia nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC , chini ya bendera ya Umoja wa Mataifa, mkuu wa mafunzo na utendaji wa kivita wa jeshi la wananchi wa Tanzania, JWTZ amezungumzia kile ambacho watafanya ili utendaji wao uendane zaidi na mazingira. Tupate maelezo zaidi kutoka Luteni Issa Mwakalambo Afisa habari wa kikosi cha 7 cha Tanzania kwenye kikosi cha kujibu mashambulizi. FIB, cha ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani DRC, MONUSCO. 

Ziara ya Meja Jenerali Alfred Kapinga hapa Beni jimboni Kivu Kaskazini ya kufuatilia utekelezaji wa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu kuleta vikundi vipya vya ulinzi wa amani, ilimpatia fursa ya kuwa na mazungumzo na kamanda wa FIB kutoka Afrika Kusini, halikadhalika walinda amani kutoka Tanzania. 

Na ndipo akaulizwa kwa nini kunafanyika mabadiliko ya vikosi? Meja Jenerali Kapinga anasema, “mabadiliko yaliyofanyika ni kupunguza baadhi ya askari kutoka vikosi vya awali na kuleta askari wapya na vikundi vipya vikiwemo vinavyoweza kufanya kazi kwa haraka zaidi yaani Quick reaction forces. Na hivyo vimeundwa na vikundi vitatu. Tanzania imeteuliwa  kuwa moja ya nchi ambazo zinaunda hivyo vikosi vya kuchukua hatua kwa haraka, na vikundi vinginevyo.”

Na yeye baada ya kufanya ziara ni kipi anaodoka nacho kwa lengo ya kuboresha utendaji?, “jeshi letu la ulinzi la wananchi wa Tanzania, limepata mafunzo katika nyanja mbalimbali, ikiwemo ardhini, angani na majini. Vilevile katika hali zote za misitu, majangwa na maeneo yote. Kwa hivyo jeshi letu lina uwezo wakufanya kazi katika mazingira mbalimbali. Lakini vilevile, jeshi letu linapokuwa limepewa majukumu maalum kama kuja DR Congo, basi jeshi linafanya mafunzo maalumu kulingana na mazingira na kule linakokwenda. Kwa mfano sasa hivi tumefika hapa DRC, tunaangalia mazingira tuone vitu gani tunatakiwa tuviongeze katika mafunzo. Hiyo tunaita mission specific training.” 

Zaidi ya yote ana kipi cha kujivunia kutoka kwa vijana wake ambao yeye ndiye mwalimu wao? Meja Jenerali Kapinga anasema, “najivunia vikosi vyangu vinafanya vizuri na Tanzania inafanya kazi vizuri na kubwa zaidi tunaona kwamba usalama wa watu wa DRC uko vizuri na ambavyo tunaleta usalama kwa nchi zote za maziwa makuu.”

Katika ziara hiyo ameambatana na Mwambata wa kijeshi katika ofisi ya mwakilishi wa kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa, nchini Marekani, Kanali George Itang’are ambaye yeye akazungumzia msingi wa Tanzania kushiriki ulinzi wa amani, “Tanzania, tumekuwa tukishirika katika shughuli za ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika kwa siku nyingi na vilevile tumeshiriki katika operesheni nyingi sana nje ya nchi. Utakumbukia Ushelisheli, Msumbiji na Comoro. Yote hayo yanaonesha mchango wa Tanzania katika kudumisha amani duniani. Kwa hiyo kushiriki mpango wa amani chini ya Umoja wa Mataifa, sisi kama mwanachama wa Umoja wa Mataifa, ni jukumu la kikatiba, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya mambo ya nje ya Tanzania.”