Udadisi wangu katika magari ulinichochea kuwa mhandisi wa magari- Francine

11 Februari 2021

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya wanawake na wasichana kwenye nyanja ya sayansi, Umoja wa Mataifa unakumbusha kuwa bado makundi hayo yanaenguliwa katika masomo na ajira za kisayansi huku msichana Francine Giramata kutoka Rwanda akielezea vile ambavyo aliamua kuzingatia ndoto yake ya kufahamu muundo wa magari kwa kina.

Ni Francine Giramata huyu kama anavyojitambulisha, mhandisi wa mitambo katika karakana ya magari aina ya Hyundai nchini Rwanda. 

Francine ni miongoni mwa wasichana wachache katika nyanja inayomilikiwa na wanaume wengi zaidi siyo tu nchini humo bali duniani kwa ujumla.

Francine amejikita katika mifumo ya elektroniki na ufungaji nyaya za magari sambamba na kutambua matatizo yake ya kimfumo.

Msichana huyu anasema tangu mtoto alivutiwa na jinsi magari yanafanya kazi na ndipo akaamua kusomea uhandisi wa magari. 

Anasema hata hivyo huwa anapata changamoto hususan pale watu wanaponiambia kuwa hii si kazi yangu bali ni kazi ya wanaume pekee. Ninakabili kazi hizo kwa kujikumbusha kuwa kila wakati ndoto yangu ilikuwa ni kufahamu mfumo wa magari na ndio maana nilisomea kazi hii kwa mapenzi makubwa na naifanya kwa utashi wangu.

Francine anasema ni vyema wasichana wakasomea masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hesabu, STEM kwa kuwa hivi sasa wanaume ndio wengi kwenye nyanja hiyo akisema,,

Hakuna ukomo wa kile ambacho wanawake wanaweza kufanya. Ushauri kwa wasichana wanaotaka kusoma STEM ni kwamba wajiamini na watambue kuwa wanaweza kufanya chochote. Ninaamini naweza na tunaweza!

Francine ni sehemu ya mradi wa mradi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF nchini Rwanda na Wizara ya Elimu nchini humo wa kuhamasisha wasichana walioko shule za msingi kuendeleza na kuchukua masomo ya STEM kuanzia shule ya msingi ili hatimaye wachanue katika nyanja za sayansi.

Kwa mujibu wa Audrey Aozulay, Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO ambao ndio waratibu wa siku hii, hata katika karne ya sasa ya 21, wanawake na wasichana bado wanaenguliwa kwenye nyanja ya sayansi kwa sababu ya jinsia yao.

Bi. Azoulay amesema “wanawake na wasichana wanapaswa kutambua kuwa wana nafasi katika sayansi, teknolojia, uhandisi na hesabu na kwamba wana haki ya kuwa sehemu ya maendeleo ya kisayansi.”
 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter