Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Suala la wakimbizi wa ndani Somalia lahitaji suluhu ya kudumu: Abdelmoula

Watoto wakiwa katika kambi ya wakimbizi wa ndani, IDPs mjini Mogadishu.
UN Photo/Stuart Price
Watoto wakiwa katika kambi ya wakimbizi wa ndani, IDPs mjini Mogadishu.

Suala la wakimbizi wa ndani Somalia lahitaji suluhu ya kudumu: Abdelmoula

Wahamiaji na Wakimbizi

Wakimbizi wa ndani nchini Somalia ni mtihani mkubwa ambao mratibu mkazi wa Umoja wa Mataifa na wa masuala ya kibinadamu nchini humo  Adam Abdelmoula, akiwa ziarani Baidoa amesema linahitaji dawa mujarabu na ya muda mrefu.

Mjini Baidoa baada ya kuwasili na kukutana na wenyeji wake  hasa kutoka Umoja wa Mataifa Bwana Abdelmoula alifunga safari hadi kwenye makazi ya maelfu ya wakimbizi wa ndani ya Hataatafor kusikiliza vilio vyao. 

Asilimia kubwa ya wakimbizi hao ni wanawake na watoto na miongoni mwao ni Bi. Fatuma Isaq Mohamed mwenye umri wa miaka 54 anayeishi kambini hapo na wanawe 10 anasema maisha ya kila siku ni changamoto kubwa. “Hapa sio nyumbani kwetu na sijui tutakuwa hapa kwa muda gani, matatizo na mahitaji yetu kambini hapa ni mengi. Tunahitaji haraka chakula na maji. Ili kuweza kuishi mara kadhaa inabidi nifanye kazi ngumu kambini hapa zinazoweza kunipatia kipato, hata hivyo sio kazi za kuaminika na hazitoshelezi kuweza kujikimu.” 

Kama walivyo maelfu wengine, Fatuma alikimbia mapigano kwenye mji wa Diinsor katika jimbo la Bay miaka minne iliyopita na tangu wakati huo yeye na wanawe wamekuwa wakiishi kambini hapa katika hali ya sintofahamu, bila ulinzi na wakati mwingine wakikosa huduma za msingi.

Mratibu mkazi Abdelmoula amesikia mlolongo wa changamoto zao kuanzia malazi duni, ukosefu wa chakula na maji, upungufu wa madawa, elimu , fursa za ajira na kwa familia nyingi tatizo la ukosefu wa utulivu. 

Wadau mbalimbali wakiwemo wahudumu kambini hapo, viongozi wa serikiali wa eneo hilo na wadau wa Umoja wa Mataifa  aliokutana nao wote wamemuelezea changamoto zilezile.  

Amewaahidi wakimbizi hao wa ndani kwamba Umoja wa Mataifa utafanya kila uwezalo kubadili maisha yao na sasa unashirikiana na serikali katika mradi wa miaka 3 unaowalenga wakimbizi wa ndani katika kusaka suluhu ya kudumu sio tu Baidoa bali pia Bosasso Puntland na Belet Weyne Hirshabelle. Ameongeza kuwa Hii ilikuwa fursa ya kipekee kuzuru Baidoa na pia kutembelea jamii za wakimbizi wa ndani na kuweza kuzungumza na spika kuhusu ni jinsi gani tunaweza kushirikiana pamoja kusaka suluhu ya kudumu kwa baadhi ya changamoto sugu ambazo zinalikabili jimbo hili la Kusini Magharibi.” 

Changamoto kubwa ni pamoja na vita vya miaka nenda rudi, mafuriko makubwa 19 na majira 17 ya ukame tangu mwaka 2000  ambazo zimeifanya Somalia kuwa moja ya nchi yenye idadi kubwa zaidi ya wakimbizi wa ndani duniani.