Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuna haja ya haraka kuzisaidia jamii zilizoathirika vibaya na ukame Somaliland:UN

Msichana anacheza na mdogo wake wa kike katika kituo cha huduma ya afya ya watoto wa uzazi huko Hargeisa, Somaliland.
UNFPA Somalia/Tobin Jones
Msichana anacheza na mdogo wake wa kike katika kituo cha huduma ya afya ya watoto wa uzazi huko Hargeisa, Somaliland.

Kuna haja ya haraka kuzisaidia jamii zilizoathirika vibaya na ukame Somaliland:UN

Msaada wa Kibinadamu

Naibu mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa na mratibu wa masuala ya kibinadamu nchini Somalia, Adam Abdelmoula, ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuzisaidia haraka jamii zilizoathirika vibaya na ukame baada ya kukamilisha ziara ya siku mbili katika maeneo yaliiyoathika zaidi Somaliland.

Katika mji wa Cunaqabad nje kidogo ya mji mkuu wa Somaliland Hargeisa, bwana Abdelmoula anawasili na timu yake ya Umoja wa Mataifa kushuhudia hali halisi ya ukame na athari zake kwa jamii hii na kuzungumza na waathirika. 

Kwa hakika hali ni mbaya dhahiri shairi na baada ya kuzungumza na wafanyakazi wa misaada wa Umoja wa Msataifa ambao wanajitahidi kukimu mahitaji ya haraka ya watu hawa ikiwemo chakula na  pia waathirika ambao wengi ni wakimbizi wa ndani, amebaini kuwa kuna ongezeko kubwa la watu waliotawanywa kutoka maeneo mengine yaliyoathirika na ukame ambao wamefika hapa Somaliland kusaka hifadhi, hali ambayo amesema inaongeza shinikizo kwa rasilimali chache zilizopo kwa jamii akisisitiza kuwa “ kuna haja ya kuongeza uwekezaji katika suluhu ya kudumu kwenye maeneo yaliyoathirika na ukame , kwani hali hii inaongeza shinikizo na  ni muhimu kuboresha ufikishaji wa huduma za kijamii katika maeneo yanayohifadhi wakimbizi wa ndani.” 

Akihitimisha ziara hiyo ya siku mbili Adam Abdelmoula ameisihi jumuiya ya kimataifa kunyoosha mkono kusaidia kwa hali na mali “ Tunachohitaji kufanya ni kuwekeza zaidi katika maeneo ya asili ya watu wa jamii hizi zilizotawanywa ili kuhakikisha wanaweza kusalia makwao kwa usalama na wakati huohuo kuboresha huduma za kijamii kwenye maeneo amnbayo yameshuhudia idadi kubwa ya watu wakiwasili kwa sababu ya ukame.” 

Kwa mwaka huu wa 2022 mipango ya kibinadamu nchini Somalia inahitaji dola bilioni 1.5 ili kuwasaidia watu milioni 5.5 walio hatarini wakiwemo milioni 1.6 wakimbizi wa ndani, milioni 3.9 ambao sio wakimbizi na watu wenye ulemavu.