Wakimbizi wa ndani milioni 2.6 wanahitaji maji, malazi na chakula Somalia:IOM

22 Oktoba 2019

Baada ya kughubikwa na vita kwa zaidi ya miongo mitatu sasa, ukame wa hivi karibuni umezidisha adha kwa mamilioni ya Wasomali ambao sasa wanahitaji huduma za msingi kama maji, malazi, huduma za afya na chakula.

Kwa mujibu wa taarifa ya shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM iliyotolewa leo kuna taarifa za kuhitajika msaada wa haraka wa mahitaji hayo ya msingi katika maeneo yaliyoathirika zaidi ikiwemo Baidoa.

Katika nusu ya kwanza ya mwaka huu 2019 sababu kuu zilizolazimisha watu kufungasha virago na kukimbia makwao Somalia ilikuwa ni usalama mdogo, ukame na mafuriko na kwa sasa kuna jumla ya watu milioni 2.6 waliosalia kuwa wakimbizi wa ndani Somalia. Kukiwa na watu milioni 15 wanaoishi nchini Somalia , milioni 5.4 kati yao sawa na asilimia 30 wanakadiriwa kutokuwa na uhakika wa chakula  huku milioni 2.2 kati yao wako katika hali mbaya ya kutojua mlo unaofuta utatoka wapi.

Zaidi ya nusu ya watu wote Somalia wanaishi katika umasikini huku kiwango kikubwa cha umasikini kikiwa miongoni mwa makazi ya wakimbizi wa ndani ambako waathirika wakubwa ni watu kutoka maeneo ya Lower Shabelle, Bakool, Bay na Sanaag na hali hiyo inaelekea katika maeneo ya Shabelle ya Kati na Banadir.

IOM inasema Baidoa mji mkuu wa jimbo la Bay ni moja ya miji inayohifadhi idadi kubwa ya wakimbizi wa ndani nchini Somalia. Hadi kufikia Septemba mwaka 2019 Baidoa imekuwa na jumla ya wakimbizi wa ndani 359,994 wanaoishi katika maeneo 435 ya mji huo.

Ali Ahmed afisa wa IOM Baidoa anasematuna watu wapya hapa wanakuja kila siku, kila wiki na pengo kubwa kwa wakimbizi hawa wapya wanaowasili ni chakula, maji na malazi, hiyo ndio changamoto kubwa”

Naye mkuu wa IOM Somalia Dyane Epstein amesema, “mahitaji ni makubwa na IOM inafanyakazi kwa pamoja na serikali, jamii, na wadau wa kimataifa ili kutoa msaada unaohitajika haraka na kuhakikisha mahitaji ya msingi yanatimizwa.”

Kwa pamoja hadi mwezi juni mwaka huu 2019 ukanda wa Mashariki na Pembbe ya Afrika umekuwa na jumla ya wakimbizi wa ndani milioni 8.1 na wengine milioni 3.5 ni wakimbizi na waomba hifadhi.

Somalia yenyewe imehifadhi wakimbizi na waomba hifadhi 17,000 ambao walipewa maskani Wogooyi Galbeed, Bari na Banadir. Wengi wa waoomba hifadhi hao wanatoka Ethiopia, Yemen na nchi zingine zikiwemo Syria, Tanzania na Eritrea.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud