Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN na AU sasa bega kwa bega!

Mlinda amani wa UNAMID aizungumza na mama wakati akipiga doria katika kambi ya Zam Zam karibu na El Fasher, Darfur Kaskazini.(Picha:UNAMID/Hamid Abdulsalam)

UN na AU sasa bega kwa bega!

Amani na Usalama

Ziara hii ya pamoja ni utekelezaji wa mpango wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na mwenyekiti wa Kamisheni ya AU Moussa Faki Mahamat wa kutaka pande mbili hizo zishirikiane katika kufanikisha ajenda zao za amani na maendeleo.

Viongozi waandamizi wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika, AU wako ziarani Sudan kwa lengo la kuangalia utendaji wa UNAMID, ambao ni ujumbe wa pamoja wa pande mbili hizo jimboni Darfur.

Viongozi hao Jean-Pierre Lacroix ambaye ni mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa na Balozi Smail Chergui ambaye ni Kamishna wa amani na usalama wa AU wanaangalia pia mfumo mpya pendekezwa wa UNAMID pamoja na changamoto zinazokumba ujumbe huo katika kutekeleza majukumu yake.

Katika kufanikisha hilo tayari wameshiriki mkutano wa utatu wa AU, Umoja wa Mataifa na serikali ya Sudan, kikiwa ni kikao cha 25 kinachoratibu utendaji wa UNAMID.
Halikadhalika wamekuwa na mazungumzo na pande mbalimbali nchini Sudan kuhusu hali ilivyo huko Darfur.

Mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani kwenye UN Jean-Pierre Lacroix (wa pili kutoka kushoto) na Kamishna wa amani na usalama wa AU Smail Chergui (wa pili kutoka kulia) baada ya kulakiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan Ibrahim Ghandour (Kulia).
Ashraf Eissa/UNAMID

Baada ya ziara yao huko Sudan, siku ya Jumanne tarehe 10 Bwana Lacroix na Balozi Chergui wataelekea Bangui, mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR ambako watajidili ushirikiano kati ya AU na UN katika kusaka suluhu ya kudumu ya kisiasa kwenye mzozo unaoendelea nchini humo.

Wawili hao wataongoza mkutano wa kwanza wa kundi la kimataifa la usaidizi kwa CAR kwa lengo la kushawishi jamii ya kimataifa ijihusishe tena na mchakato wa amani na kusaidia mahitaji ya dharura ya kibinadamu kwa mamilioni ya watu nchini humo.

Hatimaye Bwana Lacroix na Balozi Chergui wataelekea Addis Ababa Ethiopia ambako tarehe 13 mwezi huu watazungumza kwenye kikao cha Baraza la Amani na Usalama la AU na kukutana na viongozi waandamizi wa chombo hicho.