Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN tayoa wito wa kurejea kuokoa watu Mediterranea baada ya 43 kupoteza maisha Libya

Wahamiaji wakiokolewa baada ya kuvuka bahari ya Mediteranea.
PICHA: IOM/Francesco Malavolta (maktaba)
Wahamiaji wakiokolewa baada ya kuvuka bahari ya Mediteranea.

UN tayoa wito wa kurejea kuokoa watu Mediterranea baada ya 43 kupoteza maisha Libya

Wahamiaji na Wakimbizi

Kufuatia ajali nyingine ya boti iliyokatili maisha ya watu 43 siku ya Jumatatu kwenye pwani ya Libya, mashirika ya Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM na lile la kuhudumia wakimbizi UNHCR yametoa wito kwa nchi kurejea operesheni za kuwasaka na kuwaokoa watu kwenye bahari hiyo.

Katika taarifa yao ya pamoja iliyotolewa leo Jumatano mashirika hayo mawili yameelezea huzuni yao kwa ajali hiyo mbaya ambayo ni ya kwanza kwa mwaka huu wa 2021 katika Mediterrania ya Kati.

Boti hiyo imearifiwa kuzama kutokana kuchafuka kwa bahari wakati ambapo injini ilizima saa chache tu baada ya kuondoka mjini Zawra Libya Jumanne asubuhi.

Manusura 10 ambao weni ni kutoka Cote d’Ivoire, Nigeria, Ghana na Gambia wamearifu kwamba wale waliopoteza maisha wote walikuwa ni wanaume kutoka Afrika Magharibi.

Wafanyakazi wa IOM walihusika na shughuli za uokozi wakati boti lilipozama kwenye ufukwe wa Libya.(Maktaba)
IOM/Hussein Ben Mosa
Wafanyakazi wa IOM walihusika na shughuli za uokozi wakati boti lilipozama kwenye ufukwe wa Libya.(Maktaba)

Msaada wa dharura

Manusura wamepokea msaada wa dharura ikiwemo chakula, maji na uchunguzi wa kitabibu kutoka IOM na kwa wafanyakazi wa kamati ya kimataifa ya uokozi.

Operesheni za uokozi kwenye bahari ya Mediterranea zimepungua kwa kiasi kikubwa katika miaka ya karibuni na mashirika mengi yasiyo ya kiserikali (NGO’s) yameelezwa kuulaumu Muungano wa Ulaya na nachi wanachama kwa kuongezeka kwa idadi ya vifo katika ukanda huo.

IOM na UNHCR wamerejea wito wao kwa jumuiya ya kimataifa wa kuchukua mtazamo wa haraka na ulio na mashiko kuhusu hali Mediterranea.

Mtazamo nah atua hizo ni pamoja na kuhakikisha wanaacha kuwarejesha watu katika bandari zisizo salama, kuanzisha mchakato salama na unaoaminika wa uokozi ukifuatiwa na mshikamano wa hali ya juu kutoka kwa nchi za Ulaya kwa nchi zinazopokea idadi kubwa ya watu wanaowasili.