Maiti 60 za wahamiaji zaopolewa ziwa Van Uturuki baada ya kufa maji:IOM

22 Julai 2020

Shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM limesema shughuli za uokozi zinaendelea ili kuopoa miili zaidi ya wahamiaji waliokufa maji katika ziwa Van Mashariki mwa Uturuki baada ya meli ya uvuvi iliyokuwa inawasafirisha kuzama wiki tatu zilizopita.

Timu ya uokozi ya Uturiki katika taarifa yake iliyotolewa jana Jumanne mjini Instanbul imesema hadi sasa imeshaopoa maiti 60 katika moja janga baya zaidi linalohusisha wahamiaji nchini Uturuki katika miaka ya karibuni.

IOM imesema boti hiyo ilizama usiku wa tarehe 27 Juni ikikisiwa kuwa na wahamiaji takribani 80, na vifo vilivyothibitishwa vimeongezeka tangu wakati huo huku taarifa zikisema miongoni mwa maiti zilizokwishaopolewa kuna watoto wawili.

Ajali hiyo  imetokea katika ziwa Van ambalo liko kwenye mpaka na Iran na wahamiaji walikuwa wakivuka ziwa hilo kwa kutumia boti ya uvuvi katika jaribio la kukwepa polisi kwenye vituo vya ukakuguzi barabarani kwa lengo la kuingia Magharibi mwa Uturuki.

Kwa mujibu wa duru za awali za habari baadhi ya waliofariki dunia huenda wakawa ni raia wa Afghanistan na Pakistan.

IOM imesema hivi sasa familia kutoka Afghanistan, Psakistan na Iran zimeanza kusaka taarifa ili kubaini endapo wapendwa wao ni miongoni mwa waliofariki dunia.

 

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter