Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuna matumaini ya kutokomeza ugonjwa wa mifugo wa PPR:FAO/OIE 

Kondoo wakilishwa kandoni mwa barabara Nagorno-Karabakh.
Unsplash/Lora Ohanessian
Kondoo wakilishwa kandoni mwa barabara Nagorno-Karabakh.

Kuna matumaini ya kutokomeza ugonjwa wa mifugo wa PPR:FAO/OIE 

Afya

Shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa FAO na shirikika la kimataifa la afya ya mifugo OIE, leo wamesema utokomezaji wa ugonywa wa kuambukiza unaoathiri wanyama wadogo hasa mbuzi na kondoo maarufu kama PPR unaweza kutokomezwa ifikapo 2030.

Kwa mujibu wa mashirika hayo ugojwa huo Peste des Petits ruminants (Tamka pesti depetii ruminaa) PPR  ambao unatokana na virusi na kuambukiza haraka miongoni mwa mbuzi na kondoo, kimataifa idadi ya milipuko yake imepungua kwa theluthi mbili katika miaka ya karibuni. 

Hii inadhihirisha dhamira ya jumuiya ya kimataifa katika kupambana na ugonjwa huu hatari ambao huua pia kwa kasi na hivyo kuleta matumaini ya kufikia lengo la kimataifa la kutokomeza kabisa PPR ifikapo mwaka 2030 imesema taarifa ya mashirika hayo.

FAO na OIE wamekumbusha kwamba ugonjwa huu unapozuka hukatili asilimia 30-70 ya wanyama wanaoambukizwa lakini habari njema ni kwamba hauambukizi binadamu. 

Mashirika hayo yameongeza kuwa pamoja na kwamba PPR haina athari za kimwili au kiafya kwa binadamu lakini ina athari kubwa kwa wafugaji na walaji hasa kwenye suala la uhakika wa chakula, mnepo wa jamii na maisha ya watu hao. 

Kwa mwaka 2019 takwimu za FAO zinaonyesha kuwa kimataifa kulikuwa na milipuko zaidi ya 1,200 ya PPR ikiwa imeshuka kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na milipuko zaidi ya 3,500 iliyozuka 2015. 

Kupungua huko kumeelezwa ni kutokana na kampeni kubwa ya chanjo iliyofanywa kwa zaidi ya nchi 50 duniani ambapo mbuzi na kondoo zaidi ya milioni 300 walichanjwa kati ya 2015-2018. 

Kanda mbili zinazoathirika zaidi na PPR ni Asia ambayo ilikuwa na milipuko zaidi ya asilimia 75 kati ya 2015 na 2019 na Afrika ambayo ilikuwa na asilimia 24 ya milipuko hiyo. 

Familia milioni 300 kote duniani zimeelezwa kutegemea mbuzi na kondoo kwa ajili ya chakula na kipato na endapo ugonjwa huu hautotokomezwa wako hatarini kupoteza kila kitu yamesema mashirika hayo.