Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatua za kimataifa zahitajika kuzuia kusambaa kwa mafua ya nguruwe:FAO

Homa ya nguruwe ambayo inaambukiza sana na inaweza kuwa na athari kubwa kwa wafugaji wadogo. (Maktaba Machi 2017)
IAEA/Laura Gil Martinez
Homa ya nguruwe ambayo inaambukiza sana na inaweza kuwa na athari kubwa kwa wafugaji wadogo. (Maktaba Machi 2017)

Hatua za kimataifa zahitajika kuzuia kusambaa kwa mafua ya nguruwe:FAO

Afya

Shirika la afya ya wanyama duniani OIE na shrika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo FAO leo wamezindua mkakati wa pamoja wa hatua za kimataifa za kuzuia kusambaa kwa homa ya mafua ya nguruwe ya Afrika (ASF)

Kwa mujibu wa taarifa yao ya pamoja iliyotolewa mjini Roma Italia nguruwe ni miongoni mwa nyama inayoliwa sana duniani ikiwalisha asilimia 35.6 ya nyama yote inayotumiwa, lakini katika miaka ya karibuni homa ya mafua ya nguruwe ya Afrika (ASF) ambayo inaweza kusababisha vifo vya nguruwe kwa asilimia 100 imekuwa ni changamoto kubwa kwa sekta ya nguruwe.

Mashirika hayo yanasema homa hiyo imeshasababisha hasara kubwa ya kiuchumi na sasa maeneo yanayoendelea kuathirika ni Afrika, Asia, Pasifiki na Ulaya na hakuna chanjo yoyote inayofanya kazi huku ugonjwa huo ukisababisha sio tu kufa kwa nguruwe na kuhatarisha afya ya wanyama bali pia unaathiri kwa kiasi kikubwa uchumi na maisha ya wakulima.

Akizungumzia hatari ya homa hiyo ya mafua ya nguruwe Dkt. Matthew Stone mkurugenzi msaidizi wa viwango vya kimataifa na sayansi katika shirika la OIE amesema Leo hii nchi 51 zimeathirika na homa ya mafua ya nguruwe ya Afrika wakati huu mgumu ambapo dunia pia inaendelea kupambana na janga la corona au COVID-19, na hivyo kuendelea kusambaa kwa homa ya mafua ya nguruwe kunazidisha mgogoro wa kiafya, kijamii na kiuchumi.”

Ameongeza kuwa nchi nying zilizoathirika zinakabiliwa na upungufu wa rasilimali watu, fedha au ujuzi wa kiufundi kuweza kubaini, kukabiliana na kuudhibiti ugonjwa huo haraka.

Naye mkurugenzi msaidizi wa FAO Maria Helena Semedo amesema “Katika dunia hii ya utandawazi ambayo magonjwa yanaweza kusambaa kwa kasi kubwa nje ya mipaka , kushirikiana taarifa za kisayansi kwa wakati , ushirikiano wa kimataifa na kutoa taarifa ya homa hiyo ya ASF, kunahitajika ili kuzuia kusambaa zaidi katika nchi mbalimbali na kupunguza athari zake.”

FAO na OIE wametoa wito kwa nchi zote na wadau wa kote duniani kushirikiana dhidi ya ugonjwa huu hatari unaoua kwa kasi nguruwe kwa kufuata mkakati mpya wa kimataifa wa kudhibiti homa ya mafua ya nguruwe ya Afrika (ASF) uliozinduliwa leo.