Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ofisi ya haki za binadamu ya UN yaelezea wasiwasi kufuatia ghasia zinazoendelea CAR

MINUSCA wametuma vikosi vya polisi katika mji mkuu wa CAR, Bangui na viunga vyake kufuatia mashambulizi yaliyofanywa na makundi yenye silaha kaskazini magharibi mwa mji.
MINUSCA/Hervé Serefio
MINUSCA wametuma vikosi vya polisi katika mji mkuu wa CAR, Bangui na viunga vyake kufuatia mashambulizi yaliyofanywa na makundi yenye silaha kaskazini magharibi mwa mji.

Ofisi ya haki za binadamu ya UN yaelezea wasiwasi kufuatia ghasia zinazoendelea CAR

Haki za binadamu

Siku chache kabla ya uchaguzi nchini Jamhuri ya Afrika ya kati, CAR, unaotarajiwa tarehe 27 Desemba,  ghasia zimekuwa tishio kubwa kwa usalama wa raia na kuheshimiwa haki ya kupiga kura. 

Msemjai wa ofisi ya haki za binadamu ya umoja wa Mataifa, OHCHR, Liz Throssel,  anasema wana wasi mkubwa kutokana na kusambaa ghasia zitokanazo na uchochezi ambapo watu wamelazimika kuhama makwao hadi kuingia katika nchi jirani. 

Kumekuwa na ripoti kadhaa siku za hivi karibuni za mashambulizi dhidi ya vikosi vya usalama, wagombea kwenye uchaguzi na maafisa wa uchaguzi. Mapigano kati ya makundi yenye silaha na vikosi vya usalama yametokea katika maeneo kadhaa yakiwemo yale yaliyo karibu na mji mkuu Bangui.

"Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa inaungana na Katibu Mkuu António Guterres kutoa wito kwa pande zote vikiwemo vikosi va ulinzi na makundi yenye silaha na pia vikosi vya kigeni kwamba wanahitaji kuheshimu sheria za haki za binadamu na kwamba usalama kwa raia ni muhimu." Ameeleza msemaji huyo wa OHCHR. 

Wadau kwenye makubaliano ya kisiasa ya mwezi Februria 2019 wakiwemo wanasiasa na makundi yenye silaha wanahitajika kuheshimu makubaliano yao ya kulinda haki za binadamu na wasitumie ghasia kutatua migogoro.