Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ulinzi tulionao kwa wakati huu ni chanjo – Walinda amani Jamhuri ya Afrika ya kati 

Kampeni ya chanjo dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 kwa walinda amani wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR.
MINUSCA - Herve Cyriaque Serefio
Kampeni ya chanjo dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 kwa walinda amani wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR.

Ulinzi tulionao kwa wakati huu ni chanjo – Walinda amani Jamhuri ya Afrika ya kati 

Afya

Kampeni ya chanjo dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 kwa walinda amani wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR imezinduliwa mwanzoni wa wiki hii kwa kuwa walinda amani ni moja ya makundi ya kipaumbele. 

Wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa walioko mstari wa mbele ni miongoni mwa makundi ya kipaumbele ya chanjo dhidi ya COVID-19 kwa sababu ya ukaribu wao kwa watu walio katika mazingira hatarishi ambao wanawalinda katika majukumu yao ya ulinzi wa amani. 

Katika mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya kati, Bangui, katika hospitali ya Umoja wa Mataifa, walinda amani wa Ujumbe wa kuweka amani nchini CAR, MINUSCA, wanaonekana wakisubiri nje wakati chanjo za Astra Zeneca zinaadaliwa na huku wengine wakijiorodhesha.  

Naibu Kamanda wa Kikosi cha MINUSCA, Jenerali Paulo Emanuel Maia Pereira anakuwa mfanyakazi wa kwanza kupokea dozi ya kwanza ya  chanjo ya Astra Zeneca. Jenerali Pereira baada ya kuchanjwa, anasema, “Kikosi kiko hapa kutimiza jukumu lake na kwa hiyo lazima tujilinde. Ulinzi tulionao kwa wakati huu ni chanjo. Kwa upande wangu, kama mtiririko wa amri, ninatoa mfano kwa kuja hapa kuonesha kila mtu kwamba chanjo ndiyo njia pekee ya ulinzi tuliyonayo.” 

Mwingine ambaye amechanjwa ni Milan Dawo Mkuu wa Usalama wa Barabara katika MINUSCA, anasema,  "Ni muhimu sana kwetu kwa sababu hatuwezi kuendelea kuokoa watu ikiwa hatuko salama. Kujilinda ni bora kwa wote, nadhani tutakuwa katika hali nzuri ya kutulinda tunapokuwa na afya njema. Ninataka kuhimiza wafanyakazi wote wa kimataifa kumaliza hofu yao, kujitokeza na kuchukua chanjo hii.” 

Shehena ya kwanza ya chanjo iliyopokelewa na MINUSCA, itatumika kuchanja wafanyakazi wa MINUSCA, wakiwemo walinda amani, mashirika ya Umoja wa Mataifa na mashirika ya kimataifa, wafanyakazi wa kitaifa, na familia zao.