Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuepushe mapigano CAR, hali ni tete- Zeid

Wakimbizi wa ndani 698 kutoka kambi ya muda karibu na kituo cha ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini CAR wanahamishwa. Picha: IOM

Tuepushe mapigano CAR, hali ni tete- Zeid

Amani na Usalama

Ghasia zinazidi kupamba moto nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR jambo ambalo linamtia hofu kubwa Kamishna Mkuu wa haki za binadamu, Zeid Ra’ad Al Hussein.

Kamishna huyo amenukuliwa leo kupitia taarifa ya ofisi yake akisema kuwa kinachomtia hofu zaidi ni kauli za chuki zinazotolewa kwa misingi ya dini pamoja na mauaji  ya hivi karibuni kwenye mji mkuu Bangui.

Amesema mauaji ya wiki iliyopita ya watu 22 yaliyotokea baada ya watu wenye silaha kuvamia kanisa yanadhihirisha ni kwa jinsi gani hali ni tete nchini CAR.

Bwana Zeid amesema vitendo hivyo vinachochea visasi kutoka jamii ya wakristo akisema sasa mapigano yameenea na watu wanashambulia makazi, hospitali , makanisa na misikiti.

Amesema kwa kuwa uchochezi huo unafanyika pia kupitia mitandao ya kijamii, ana hofu kuwa mapigano kama ya wiki iliyopita yanaweza kuenea maeneo mengine kwa kasi kubwa.

Kamishna Zeid ametoa wito kwa pande husika kitaiaf na kimataifa kuchukua hatua thabiti kuzuia mashabulizi kama hayo na ukiukwaji wa haki za binadamu.

Amesisitiza kuwa ghasia za hivi karibuni katu zisiruhusiwe kuteketeza mchakato wa amani unaopigiwa shime na Muungano wa Afrika.