Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wahitimu wa mafunzo ya polisi CAR zingatie mlichofundishwa- MINUSCA

Maafisa polisi kutoka ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini  Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR wakiwa kwenye doria mjini Bouar nchini humo.
MINUSCA/Hervé Serefio
Maafisa polisi kutoka ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR wakiwa kwenye doria mjini Bouar nchini humo.

Wahitimu wa mafunzo ya polisi CAR zingatie mlichofundishwa- MINUSCA

Amani na Usalama

Nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR jumla ya polisi 380 wakiwemo maafisa wa polisi wamehitimu mafunzo ya mwezi mmoja yenye lengo la kuimarisha uwezo wao wa kulinda amani na utulivu wa umma.

Yakiwa yameendeshwa na ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu nchini CAR, MINUSCA, mafunzo hayo yamewezesha askari hao kupata stadi kama vile za sheria hususan kwenye kutuliza ghasia, kukamata watuhumiwa wa uhalifu  wakiwemo watoto wadogo, kutuliza na kudhibiti umati wa watu wenye hasira kali pamoja na kuimarisha usalama kwenye maeneo ya vijijini.

Akizungumza kwenye mji mkuu Bangui wakati wa ufungaji wa mafunzo hayo yaliyodhaminiwa na MINUSCA, mkuu wa polisi kwenye ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa Kanali Ossama El Moghazy amesema, “ninyi ni moja ya alama za serikali na vitendo vyenu vyote vinapaswa kuzingatia viwango vya kimataifa wakati mnadhibiti maandamano au migomo.”

Miongozo ambayo ilitumika kwenye mafunzo hayo imezingatia kanuni za kimataifa na hivyo Kanali El Moghazy amewasihi wazingatie ili wawe na ueledi kwenye kazi yao na wakati huo huo watakuwa wanaheshimu haki za binadamu.

Kanali Jean-Claude Matongo ambaye ni Waziri wa mambo ya ndani na usalama wa  umma akizungumza kwenye hafla hiyo amekumbusha wahitimu kuwa, “mmepokea funguo zote za jukumu lenu la uaskari wa kusimamia sheria hususan utulivu wa umma.

Mchakato wa mafunzo haya ulianza mwaka 2016 na wahitimu hawa wa hivi karibuni zaidi  wanasubiri kusambazwa kwenye maeneo mbalimbali ya CAR ili kusaidia kuimarisha amani.