Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNCDF na wadau Tanzania waondolea wakulima hofu ya kupata pembejeo 

Pembejeo zinazotumika na wakulima huko Kigoma, Tanzania.
UNCDF/Emmanuel Lukwaro
Pembejeo zinazotumika na wakulima huko Kigoma, Tanzania.

UNCDF na wadau Tanzania waondolea wakulima hofu ya kupata pembejeo 

Ukuaji wa Kiuchumi

Nchini Tanzania Umoja wa Mataifa kupitia shirika lake la mitaji UNCDF na wadau wamezindua mpango wa kutumia teknolojia ya simu ya kiganjani kumwezesha mkulima mkoani Kigoma magharibi mwa taifa hilo kuweza kupata pembejeo za kilimo wakati anapohitaji. 

Mfumo huu ambao unaendeshawa na kampuni ya DMA kwa kushirikiana na  UNCDF chini ya Programu ya Pamoja Kigoma (KJP) unalenga pia kuimarisha mtandao wa mawakala wa pembejeo vijijini au Village Digital Agents (VIDA Local)  na kuwaunganisha wanavikundi na watoa huduma za kifedha kama vile benki na kampuni za simu. 

UNCDF inasema kuwa mfumo huo wa kidigitali utamrahisishia pia mkulima kupata taarifa muhimu za pembejeo ikiwa ni pamoja na bei kwa kutumia simu ya mkononi. 

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango huo wilayani Kasulu, mratibu wa mradi UNCDF Emmanuel Lukwaro amesema, “kwanza unakwenda kumsaidia mkulima kwanza kuwa na uhakika wa kuweka akiba kwa ajili ya pembejeo, akiba ambayo atakuwa anaweka kidogo kidogo kupitia mfumo wa simu yake ya kawaida kwa mwaka mzima hadi unapofika msimu wa kilimo inakuwa akiba yake imeshakamilika. Lakini pia utakuwa unamhakikishia  kupata mbolea bora kwa maana kwamba DMA watakuwa wanafanya kazi  na wasambazaji wanaotambuliwa na serikali na mbolea itamfikia moja kwa moja kutoka kwa wasambazaji hao.” 

Bwana Lukwaro amesema awali kulikuwepo na changamoto ya baadhiya pembejeo kutokuwa na ubora. Lakini mfumo huu utamhakikisha ubora. 

Halikadhalika pembejeo zitafika kwa wakati akifafanua kuwa, “iwapo mbolea ya kupandia inamfikia wakati mazao tayari yako ardhini, hiyo haina faida tena. Vile vile pembejeo kumfikia mkulima wakati lakini hana fedha, inakuwa haina maana kwa sababu hatoinunua na hataitumia, lakini mfumo huo unamhakikishia vitu hivyo vinakwenda sambamba. Jambo lingine ni urahisi wa pembejeo.” 

Amesema mara nyingi serikali inakuwa imetoa bei elekezi ya pembejeo lakini gharama za usafirishaji huongeza bei. 

Hata hivyo kupitia mfumo huu mkulima atafikishiwa pembejeo pale pale alipo kijijini kupitia mawakala wa kidijitali kwa bei elekezi ya serikali kwenye wilaya husika. 

Wakulima nao wapaza sauti 

Wakulima nao wamepaza sauti na miongoni mwao ni Josephina Nyongoli wa kijii cha Kitahana kikundi cha Tushirikiane wilayani Kibondo, amesema  kilimo akiba kitamwezesha kuweka akiba kidogo kidogo kwa msimu ujao ambapo akiba itamwezesha kununua pembejeo. 

Amesema atakapokuwa ameweka akiba itamwezesha msimu ukifika kutokubabaika kusaka akiba kununua pembejeo kwa kuwa “awali mbolea ilikuwa ikifika tunashindwa kununua kwa wakati kwa sababu hatukuwa na akiba.” 

Amos Ndalaba ni msimamizi wa kikundi cha kuweka na kukopa cha Kamende wilayani Kibondo na anasema, “kupitia mradi huu nimejifunza namna gani ya kuweka akiba hata kama ni shilingi 500 katika mfuko wa akiba ya pembejeo. Mfuko wa pembejeo unanisaidia kuniandaa katika msimu wa kilimo ujao ili nipate pembejeo kwa uepesi. Pembejeo za kilimo kama vile mbegu na mbolea.”