Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nasi ni kama dagaa, tunakwenda pamoja ili tuweze kustawi- Kazi Women Group 

Mwanamke nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC akiwa amebeba dagaa
UN Photo/Abel Kavanagh
Mwanamke nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC akiwa amebeba dagaa

Nasi ni kama dagaa, tunakwenda pamoja ili tuweze kustawi- Kazi Women Group 

Ukuaji wa Kiuchumi

Maisha yangu yote sijawahi kuona dagaa akiogelea mwenyewe, mara zote huenda pamoja kwenye kundi hata kwenye giza, wakisaka si tu mlo wa siku, bali kustawi! Vivyo hivyo kikundi cha wanawake cha Kazi Women Group cha mkoani Kigoma cha kuchakata na kuongeza thamani kwa dagaa. 

Flora Fundi ambaye ni katibu wa kikundi cha Kazi Women Group chenye hisa katika kampuni ya Petro and Sons ya mkoani Kigoma ya kuchakata na kuongeza thamani ya dagaa anasema wao waliamua kufuata nadharia hiyo ya dagaa ili waweze kustawi. 

Mradi wa kikundi hiki ni sehemu ya mradi wa pamoja wa Kigoma, KJP unaotekelezwa na shirika la Umoja wa Mataifa la mitaji, UNCDF kwa ushirikiano na serikali ya Tanzania. Akifananisha safari yao na dagaa, Flora anasema, “nasi wanawake wa Kazi Women Group tumejiunga pamoja kuchapa kazi, na sisi hatutaki kuishi tu, tunataka kukua, tunata  kustawi na tunatak akujikomboa kutoka katika umaskini” 

Mradi wa KJP uliwawezesha vipi? 

Kupitia KJP waliwezeshwa kwa kuwa “mashine bora za kisasa zimetuwezesha kukausha dagaa wengi zaidi, na tunweza kuzikausha zikawa bora na zikaweza kudumu kwa muda mrefu. Sasa tunaweza kuwa na mzigo mkubwa hata nje ya msimu wa dagaa. Soko linapobadilika, tunaweza kubadilika nalo. 

Na mafanikio yao ni dhahiri kwa kuwa Flora anasema“leo hii sisi hatuogelei tena gizani tukitafuta mlo wa siku moja. Njia yetu ina mwangaza na hatma yetu iko dhahiri kabisa, tunastawi sasa. Safari yetu imefaidishwa na wadau wanaoelewa kuwa safari siyo kitu cha siku moja, namna pekee ya kufika mbali ni kwenda kwa pamoja na kufanikiwa.” 

Programu ya pamoja kwa mkoa wa Kigoma ilianza mwaka 2017 na mashirika ya Umoja wa Mataifa yanayohusika ni pamoja na lile chakula na kilimo, FAO, mpango wa chakula, WFP, kituo cha biashara cha kimataifa, ITC na lile la maendeleo ya mitaji, UNCDF.