Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nashukuru FAO badala ya debe 5 za mahindi sasa navuna magunia 30- Mkulima 

Mkulima akikagua mahindi yaliyozingatia mbinu bora za kilimo
FAO Tanzania
Mkulima akikagua mahindi yaliyozingatia mbinu bora za kilimo

Nashukuru FAO badala ya debe 5 za mahindi sasa navuna magunia 30- Mkulima 

Ukuaji wa Kiuchumi

Kuelekea mkutano wa Umoja Mataifa kuhusu mifumo endelevu ya vyakula kuanzia shambani hadi mezani, huko mkoani Kigoma nchini Tanzania mradi wa pamoja Kigoma KJP unaoendeshwa kwa pamoja na serikali na mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo lile la chakula na kilimo, FAO umezidi kuwajengea kujiamini wakulima kwa kuwa hivi sasa kilimo chao kinahimili mabadiliko ya tabianchi na kiwango cha mavuno kimeongezeka bila uchovu ikilinganishwa na awali.

Miongoni mwa wakulima hao ni Elizabeth Matanya ambaye ni mkulima kiongozi kutoka Kibondo mkoani Kigoma ambaye yeye alipata mafunzo ya kilimo hifadhi cha mihogo, maharagwe na mahindi.

Bi. Matanya anasema, “kwa mradi huu nimefaidika kujifunza kupanda kwa kutumia mstari hadi mstari ambapo nimepanda mahindi na maharagwe katikati. Nimepata mazao kwa sehemu zote mbili mahindi gunia 30 na maharage gunia 10. Kipindi cha nyuma ambako sikutumia mistari au mbinu bora za kilimo, eka moja nilipata debe 5 za mahindi na maharagwe debe moja na nusu."

Eugene Hengama akiwa kwenye shamba lake la mahindi akafafanua walichofundishwa ya kwamba katika mahindi wanalaza tu mabua ili hatimaye yaoze na atakapokata mashimo kwa ajili ya upanzi wa msimu ujao, “hapa panakuwa pameshajiwekea mbolea kutokana na majani yaliyoozea hapa.”

Bwana Hengama anasema sasa mavuno yameongezeka, halikadhalika kipato “watoto wangu wote wanasoma na nilikuwa sina baiskeli, nimeshanunua na sasa pia nimenunua pikipiki.”

Kwa wakulima wa mihogo nao hawakuachwa nyuma kama asemavyo Japhet Magwala wa kikundi cha Tushirikiane. “Tumeelimishwa namna ya kutambua ugonjwa wa batobato kwenye mihogo. Hivyo tunaweza kutambua iwapo shamba langu lina ugonjwa wa batobato au la.

Mavuno ya mihogo huko Kigoma Tanzania
FAO Tanzania
Mavuno ya mihogo huko Kigoma Tanzania

Advera naye anaunga mkono akiongezea suala la faida ya kilimo na ufugaji akisema, “nami ni mfugaji wa nguruwe. Halikadhalika nafuga kuku hivyo nikitoka nyumbani naweza kuwaachia watoto mayai waweze kula kwa afya yao. Pia nimejifunza kutumia samadi ya nguruwe kwa ajili ya kupikia kwenye jiko.”

Mafunzo ya FAO yamejengea uwezo wakulima kutambua udongo hai na hoi kama asemavyo Jackson Ntaziha akiwa na kifaa cha kupimia udongo kwa kuwa wanafahamu udongo wenye asidi au la na hivyo wana uhakika wa kupata mavuno mengi kwa kutumia udongo bora.

Kwa mujibu Albert Fatakanwa ambaye ni afisa kiungo wa mradi wa KJP wilayani Kibondo, mradi umekuwa na manufaa siyo tu kwa wakulima bali pia halmashauri. “Uzalishaji umeongezeka ambapo sasa kupitia uzalishaji huu hata mapato ya halmashauri  yanaongezeka kwa sababu sehemu kubwa ya mapato ya halmashauri yanategemea mazao ya kilimo.”