WFP yaendelea kutoa chakula kwa wakimbizi wanaovuka kuingia Sudan wakitokea Tigray  

Wakimbizi waliowasili kutoka Tigray Ethiopia wakileta msaada kwa ajili ya kukarabati makazi kambi ya Raquba, Kassal, Sudan.
UNFPA/Sufian Abdul-Mouty
Wakimbizi waliowasili kutoka Tigray Ethiopia wakileta msaada kwa ajili ya kukarabati makazi kambi ya Raquba, Kassal, Sudan.

WFP yaendelea kutoa chakula kwa wakimbizi wanaovuka kuingia Sudan wakitokea Tigray  

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa, WFP, hii leo mjini Geneva Uswisi limeeleza kuwa  hadi kufikia sasa limeweka vituo sita vya usambazaji wa uhifadhi wa chakula na misaada mingine muhimu ya kibinadamu kwa wakimbizi wanapohamia katika kambi mbalimbali nchini Sudan.  

WFP pia imesema inasafirisha wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu kwenda kwenye kambi zinazosimamiwa na shirika la ndege la Umoja wa Mataifa UNHAS. WFP imeweka tayari meli mbili za mafuta ili kutoa huduma kwa WFP na mashirika mengine. 

WFP imetuma chakula cha kutosha kulisha watu 60,000 kwa mwezi mmoja. Hata hivyo, chakula hicho kilikopwa kutoka katika mipango mingine ya WFP iliyopo.   

Shirika hilo hadi sasa limewafikia zaidi ya watu 48,000 na mgao wa kila mwezi, biskuti za kuongeza nguvu mwili kwa wakimbizi wanaosafiri au chakula moto ambacho hutolewa karibu na mpaka. 

 “Kuingia kwa watu wapya wanaowasili kutatatiza uwezo wa WFP kushughulikia mahitaji yaliyopo nchini Sudan wakati inakabiliana na mizozo mingi nchini kote.” Imesema WFP. 

Shirika hilo limetoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kwamba lazima iingile ili kukabiliana na hali hii wakati ghasia zinaendelea. “Tunatoa wito kwa wafadhili kuchangia ukarimu, ili tuweze kuokoa maisha katika shida hii.” Imesisitiza WFP. 

WFP inakabiliwa na upungufu wa dola za kimarekani milioni 153 kwa miezi sita ijayo kwa operesheni zake kukidhi mahitaji ya chakula kwa ajili ya walio hatarini kote nchini Sudan, pamoja na dola za kimarekani milioni 14.8 kwa wakimbizi wapya wa Ethiopia, dola za kimarekani milioni 3.8 kuongeza idadi ya ndege za UNHAS kuelekea mashariki mwa Sudan, na dola za kimarekani 750,000 kwa ukarabati wa barabara ili wajibu waweze kufika maeneo ya mbali ambapo wakimbizi wanafika.