Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO Tanzania yawapatia wakulima kifaa cha kupima afya ya udongo 

Kifaa cha kupima udongo.
FAO Tanzania
Kifaa cha kupima udongo.

FAO Tanzania yawapatia wakulima kifaa cha kupima afya ya udongo 

Ukuaji wa Kiuchumi

Hoja ya umuhimu wa kutunza bayonuai ya udongo, ambayo ni maudhui ya siku ya udongo duniani, inayoadhimishwa tarehe 5 mwezi desemba mwaka huu ni moja ya mafunzo waliyopatiwa wakulima wawezeshaji nchini Tanzania. 

Mafunzo hayo yametolewa na shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) kupitia mradi wa pamoja wa Kigoma (KJP) kwa wakulima hao wawezeshaji mkoani Kigoma ili kuhakikisha mashamba yao yana udongo hai kwa ajili ya uzalishaji wa mazao bora. 

Assumpta Massoi/UNNewsKiswahili
Habari za UN- Kipima udongo!!

 

Jonas Ntazia, mmoja wa wanakikundi cha Umoja kutoka kata ya Kitahana Wilayani Kibondo mkoani Kigoma amesema “katika kuitambua afya ya udongo yeye pamoja na wakulima wenzake walipatiwa kifaa maalumu cha kuitambua afya ya udongo katika ngazi ya shamba na kumuwezesha mkulima kufanya maamuzi sahihi ya hatua za kuchukua kabla ya kuanza msimu wa kilimo.” 

Kifaa hicho kimewawezesha kutambua hali halisi ya udongo, mapungufu ya udongo na mahitaji ya udongo ili kuboresha afya ya udongo huo. 

Akizungumzia manufaa yaliyopatikana Bwana Ntaziha amesema “ni pamoja na kupungua gharama za uendeshaji katika kilimo hasa zile zitokanazo na manunuzi ya mbolea kwani sasa hivi wakulima wananunua mbolea kwa mahitaji ya shamba na sio kiholela.” 

Eneo la wamasai nchini Tanzania limekumbwa na kiwango kikubwa cha ongezeko la mmomonyoko wa udongo
University of Plymouth/Carey Marks
Eneo la wamasai nchini Tanzania limekumbwa na kiwango kikubwa cha ongezeko la mmomonyoko wa udongo

Hasara za udongo usio na afya 

Udongo usio na afya maana yake ni udongo mfu! Ili kuurudishia uhai udongo mkulima anahitajika kuongeza virutubisho mbalimbali ikiwemo Naitrojeni, Potasiyamu na Fosiforasi.  

Hivi ni virutubisho muhimu katika udongo ambavyo vinasaidia mmea kukua vizuri. Hata hivyo vipo virutubisho vingine ambavyo huchangamsha udongo kwa kutoa nafasi ya viumbe mbalimbali kumen’genya udongo na kuruhusu uwepo wa viumbe vingi rafiki wa udongo na mimea aina mbalimbali ambayo kwa pamoja huchangia ongezeko la bioanuai.

Akizungumza faida za mafunzo ya FAO, Mratibu wa Mradi wa Pamoja wa Kigoma Martine Kapaya amesema, “mbali na mbolea za viwandani kama vile NPK, DAP, UREA na CAN, wakulima wamenufaika pia na matumizi ya samadi zitokanazo na wanyama na pia mbolea vunde ambazo zinachangia kwa kiasi kikubwa kuongeza uhai wa udongo na viumbe mbalimbali kushamiri.” 

Halikadhalika amesema wakulima wamejifunza pia mbinu sahihi za kilimo kama vile matumizi ya matandazo, makinga maji na kilimo hifadhi.