Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakulima washauriwa kufuga nyuki ili kupunguza gharama za kilimo

Mizinga ya nyuki ya kisasa, ijulikanayo kama Tanzania Top Bar Hives ikiwa imetengenezwa na mfugaji aliyepatiwa mafunzo na FAO kupitia KJP.
FAO Tanzania
Mizinga ya nyuki ya kisasa, ijulikanayo kama Tanzania Top Bar Hives ikiwa imetengenezwa na mfugaji aliyepatiwa mafunzo na FAO kupitia KJP.

Wakulima washauriwa kufuga nyuki ili kupunguza gharama za kilimo

Ukuaji wa Kiuchumi

Tarehe 20 mwezi mei kila mwaka ni siku ya nyuki duniani na kauli mbiu ya mwaka huu ni “Nyuki wana mchango, harakati za kujikwamua upya zisisahau nyuki” ikiangazia mwanzo mpya wa jamii baada ya kukumbwa na janga la corona au COVID19 lisisahau kuweka mazingira mazuri ya nyuki kuzaliana.

Kauli mbiu hii pia inalenga kuhamasisha ulinzi wa makazi ya Nyuki kwani wanasaidia uwepo wa chakula sababu Nyuki huchambusha mbegu ambazo baadae huzaa matunda ambayo hutumika kama chakula cha binadamu na Wanyama.

Leah Mushi amezungumza na mkufunzi na mnufaika wa mafunzo yaliyoendeshwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linalojihusisha na chakula na kilimo FAO mkoani Kigoma katika Shamba darasa la Mati Mitindo ili kufahamu namna wanavyohakikisha ufugaji nyuki unaendana na uimarishaji wa shughuli za kilimo.

Shughuli za ufundishaji zikiendelea katika shamba darasa la ufugaji nyuki kisasa akionekana Eliasi Lubimbi akiwa na wanafunzi wake wawili  nakujitambulisha yeye ni mtaalamu wa ufugaji nyuki.

“Katika eneo hili la ufugaji nyuki tuna kituo maalum cha kufundisha wafugaji nyuki kutengeneza mizinga ya kisasa, mizinga yote ya kisasa inayoonekana katika kituo chetu, imetengenezwa na wafugaji wenyewe kwakushirikiana na mafundi seremala waliopo katika eneo hili ambao tuliwapatia mafunzo na ipo tayari kupelekwa mashambani kwa ajili ya matumizi. kazi yetu kubwa ni kuwaelekeza mafundi seremala kutengeneza mizinga mikubwa na ya kati ili iweze kupatikana hapa kuliko wakulima kwenda kuitafuta katika sehemu za mbali sana."

Sio kutengeneza mizinga tu, bali mafunzo ya namna mbalimbali za kutega mizinga pia yanatolewa.

“Kuna aina mbalimbali za kutundika mizinga, kuna kutundika kwenye miti, kuna ya kuweka kwenye meza na majukwaa, mfano mmoja ni kama mizinga hii ambayo tumeitundika juu ya mti , kwanamna hii inasaidia katika shughuli nzima ya utunzaji wa mazingira lakini kazi kubwa tunayoitarajia hapa ni nyuki hawa kurutubisha mazao yetu mashambani katika mashamba yaliyopo karibu na shamba darasa.”

Kwa wale wanaojishughulisha na kilimo pekee, Elias anasema iwapo watataka kuongeza thamani na kupunguza gharama, basi wahakikishe wanafuga nyuki pia katika mashamba yao.

“Ningependa kushauri wakulima na wadau kwa ujumla, kila familia inayojihusisha na kilimo angalau iwe na mizinga mitatu yenye nyuki ambapo nyuki wale watasaidia katika uchambushaji wa mazao yao, lakini kwa wakati mwingine watavuna mazao ya nyuki , haya nayo atayatumia kuuza na kupata kipato, na kipato hiki akikipata atasaidia shughuli nyingine za maendeleo ikiwemo kununua pembejeo za kilimo, kupeleka watoto shule na kununua mahitaji mengine ya familia. Lakini kazi kubwa ya nyuki wanaowekwa katika mashamba ni kusaidia uchambushaji wa mazao ya kilimo.”

FAO Tanzania tayari imefundisha zaidi ya wakulima 230 na mafundi seremala 47 mbinu za ufugaji bora wa nyuki katik vijiji mbalimbali vya wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma.