Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi wa Ethiopia sasa ni zaidi ya 43,000, Mkuu wa UNHCR atembelea Kartoum Sudan kutathimini hali.

Mtoto mkimbizi wa Ethiopia akiwa amelala kwenye kituo cha muda huko Hamdayet, Sudan.
© UNHCR/Olivier Jobard
Mtoto mkimbizi wa Ethiopia akiwa amelala kwenye kituo cha muda huko Hamdayet, Sudan.

Wakimbizi wa Ethiopia sasa ni zaidi ya 43,000, Mkuu wa UNHCR atembelea Kartoum Sudan kutathimini hali.

Wahamiaji na Wakimbizi

Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, Filippo Grandi yuko ziarani nchini Khartoum, Sudan kuangazia hali ya wakimbizi wa Ethiopia ambao hadi sasa zaidi ya 43,000 wameingia mashariki mwa Sudan wakitokea jimbo la Tigray.  

Ziara hiyo inafanyika wakati ndege iliyosheheni tani 32 ya misaada kutoka UNHCR imetua Khartoum ilihali nyingine ikitarajiwa kutua Jumaatu ikiwa na tani nyingine 100 za misaada.  

Babar Baloch ni msemaji wa UNHCR ambapo akizungumza na wanahabari mjini Geneva, USwisi hii leo amesema, “Grandi atatathmini operesheni za UNHCR na serikali za kukabili wimbi hilo jipya la wakimbizi. Mashariki mwa Sudan, UNHCR inaendelea kuimarisha juhudi zake za misaada kwa ushirikiano na kamisheni ya wakimbizi ya Sudan na mamlaka za eneo hilo wakati huu ambapo kuna changamoto kubwa za vifaa.” 

Mashariki mwa Sudan, UNHCR inasema inaendelea kuimarisha juhudi zake za kutoa misaada pamoja na Kamisheni ya wakimbizi ya Sudan na mamlaka za mitaa katikati ya changamoto ngumu za vifaa. 

 “Misaada inahamasishwa kusaidia wakimbizi karibu nusu yao wakiewa ni watoto. Mashirika ya misaada ya kibinadamu yanaendelea kuchangia makazi na vifaa vingine kusaidia wakimbizi lakini rasilimali zaidi zinahitajika na Sudan inahitaji msaada wa kimataifa haraka.” Ameeleza Msemaji wa UNHCR, Babar Baloch.  

UNHCR imesaidia kuhamisha wakimbizi takribani 10,000 katika eneo la Um Rakuba, kilomita 70 zaidi kutoka mpakani kuingia ndani ya Sudan, wakati kazi ikiendelea kuweka makazi na kuboresha huduma. 

Huduma za ufuatiliaji wa familia zimeanzishwa na hizi tayari zimeunganisha wakimbizi wengi waliotenganishwa. 

UNHCR imeeleza kuwa asubuhi ya leo, ndege iliyobeba tani 32 za misaada ya dharura ya UNHCR kutoka katika hifadhi ya shirika hilo huko Dubai imetua Khartoum. Shehena nyingine imepangwa kuondoka Dubai Jumatatu na tani 100 za vitu vya ziada vya misaada. Kuna mpango wa kupeleka jumla ya shehena nne kwenda kuwasasaidia wakimbizi hao.  

Babar Baloch akielezea kilichomo katika shehena ya leo amesema, "mizigo ya leo imejumuisha mablanketi 5,000, taa 4,500 za nishati ya jua, vyandarua 2,900, karatasi 200 za plastiki kwa ajili ya kujengea makazi. Shehena ya pili itabeba mahema ya familia 1,275 na maghala 10. Msaada huu utakidhi mahitaji ya makazi ya karibia zaidi ya watu 16,000. Gharama za usafirishaji wa shehena zote mbili zimelipiwa kwa ukarimu wa Serikali ya Falme za Kiarabu. " 

Ndani ya jimbo la Tigray wasiwasi unaongezeka kuhusu usalama wa raia katika mzozo, hasa katika mji mkuu wa Mekelle, ambayo ni makazi ya zaidi ya watu 500,000. 

UNHCR inaendelea kuwa na wasiwasi wakati hali ya kibinadamu ikiendelea kuwa mbaya huko Tigray, pamoja na wale waliokimbia makazi yao na kwa wakimbizi wengine 96,000 wa Eritrea ambao watakosa chakula mapema Jumatatu ikiwa huduma haziwezi kuwafikia.