Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ethiopia na Tigray rudini kwenye meza ya mazungumzo :UN

Watu wanasubiri msaada wa chakula huko Tigray, Ethiopia
© UNOCHA/Mulu Tesfay Araya
Watu wanasubiri msaada wa chakula huko Tigray, Ethiopia

Ethiopia na Tigray rudini kwenye meza ya mazungumzo :UN

Amani na Usalama

Tume ya Kimataifa ya wataalamu wa Haki za binadamu nchini Ethiopia imekasirishwa na kuzuka upya kwa uhasama kati ya serikali ya Ethiopia na chama cha Tigray People's Liberation Front tangu wiki iliyopita na kuzitaka pande zote mbili kurudi kwenye meza ya mazungumzo kwani wanaoteseka ni raia.

Taarifa iliyotolewa leo na wataalamu hao wa Haki za binadamu kutoka Geneva Uswisi imesema mapigano hayo yanazidisha ugumu wa maisha kwa raia katika eneo hilo la Togray na kuna hatari kubwa ya kuongezeka. 

“Tuna wasiwasi hasa kuhusu ripoti za vifo vya raia katika uwanja wa michezo huko Mekelle katika eneo la Tigray, na madai ya kuwalenga raia katika mashambulizi mapya huko Kobo katika eneo la Amhara.” 

Wataalamu hao wametoa wito kwa wahusika kusitisha mapigano mara moja na kurejea mchakato wa mazungumzo ambao kila mmoja ameukubali. 

“Tunazihimiza zaidi pande zote mbili kuchukua mara moja hatua zote zinazohitajika ili kuruhusu Umoja wa Mataifa na mashirika mengine kutekeleza usambazaji wa misaada ya kibinadamu huko Tigray. 

Wamehitimisha taarifa yao kwa kusema haki za binadamu, afya, na ustawi wa raia lazima ziwe kipaumbele cha juu kwa pande zote.