Homa ya kichomi huwaacha Watoto milioni 4.2 wakihaha bila oksijeni kila mwaka:Ripoti

12 Novemba 2020

Tathimini mpya iliyotolewa leo na mashirika ya kimataifa ukiwemo Umoja wa Mataifa imesema takribani watoto milioni 4.2 wa chini ya umri wa miaka mitano wanaathirika na uhaba wa hewa ya oksjeni kutokana na homa kali ya kichomi au pneumonia.  

Tathmini hiyo ya Pamoja ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF, mkakati wa fursa za afya wa Clinton (CHAI), shirika la Save the children na taasisi ya utafiti wa watoto ya Murdoch (MCRI) imesema watoto hao wanaoathirika wanatoka katika nchi 124 za kipato cha chini cha cha wastani na kuongeza kwamba usumbufu unaotokana na janga la corona au COVID-19 kwenye mhuduma za afya utatishia kuongeza pigo katika vita dhidi ya homa ya kichomi ambayo ugonjwa wa kuambukiza ambao unakatili maisha ya watoto 800,000 wa chini ya umri wa miaka mitano kila mwaka. 

Homa ya kichomi inasababishwa na bakteria, virusi au fangasi na huwafanya watoto kukosa hewa wakati mapafu yao yakiwa yamejaa maji na usaha. 

Homa kali ya kichomi inawaathiri watoto zaidi ya milioni 22 katika nchi za kipato cha chini na cha wastani kila mwaka na inaua zaidi ya kuchanganya vifo vyote vya malaria, surau na kuhara. 

Mtoto akipata chanjo dhidi ya homa ya vichomi kwenye kituo cha afya cha Makuru nchini Kenya.
© UNICEF/Shehzad Noorani
Mtoto akipata chanjo dhidi ya homa ya vichomi kwenye kituo cha afya cha Makuru nchini Kenya.

 

Pamoja na COVID-19 tusiipe kisogo pneumonia 

Mkurugenzi mtendaji wa UNICEF Henrietta fore amesema “COVID-19 imeathiri mamilioni ya watu na kusababisha changamoto kubwa zaidi kwa watoto kote duniani. Wakati dunia ikihaha kudhibiti janga hilo na athari zake kwa walio hatarini zaidi, tusifumbie macho ukweli kwamba homa ya kichomi inaendelea kukatili maisha ya watoto waidi ya 2,000 kila siku. Hewa ya oksijeni mahospitalini inaweza kusaidia kuokoa baadhi ya maisha ya watoto hawa.” 

Ameongeza kuwa oksijeni pamoja na dawa za viuavijasumu vinaweza kuwatibu Watoto wenye homa kali ya kichoni lakini katika maeneo mengi oksjeni ya kumtibu mtoto mwenye homa kali ya kichoni kwa siku 3-4 inaweza kugharimu dola 45. 

Kwa mantinki hiyo kwa familia masikini kabisa gharama hizo ni kikwazo kikubwa kwa matibabu ukichanganya na ukweli kwamba hospitali nyingi katika nchi hizo zina uhaba wa oksijeni na wahutumu wenye mafunzo ya kutoa huduma hiyo. 

 

Mtungi wa oxijeni wa kiafya
Samuel Ramos on Unsplash
Mtungi wa oxijeni wa kiafya

Uhaba wa oksijeni kwa nchi masikini 

Kwa mujibu wa tathimini hiyo mpya nchi masikini zimekuwa zikikabiliwa na uhaba mkubwa wa mifumo ya hewa ya oksjeni na vifaa hata kabla ya kuzuka kwa janga la COVID-19 lakini mahitaji makubwa ya hewa hiyo kutokana na COVID-19 yamefanya tatizo kubwa kubwa hata zaidi.  

Habari Njema ni kwamba oksjeni inaweza kusalishwa katika nchi hizo na kwa gharama nafuu. Mkurugenzi wa shirika la Save the children la Uingereza Kevin Watkins amesema “COVID-19 imedhihirisha uhaba mkubwa na vifaa na hewa ya oksjeni katika nchi masikini. Kila mwaka mamilioni ya watoto wanafikishwa hospitali katika nchi masikini wakihitaji msaada wa oksjeni. Katika sehemu kubwa Afrika ni 1tu kati ya 5 ndiye anayepata matibabu anayohitaji, wengi wanakufa kutokana na kuchoka kwa kukosa hewa ya oksjeni wanayoihitaji ili kupona.” 

Ameongeza kuwa haipaswi kuwa hivyo “wakati dunia ikihaha kuongeza upatikanaji wa oksjeni kwa ajili ya waathirika wa COVID-19 na homa ya kichoni , ni lazima huduma hiyo ifike ambako ni vigumu kufikiwa, iwe bure kwa kila mtu na iwe endelevu. Endapo tutajikita tu na utatuzi wa muda mfupi tunajiweka katika hatari ya kukosa fursa ya kuokoa maisha kwa vizazi vijavyo.” 

Naye Dkt. Iain Barton mwenyekiti na mkurugenzi mtendaji wa CHAI amesema “Kuzisaidia nchi kujenga mnepo wa mifumo ya kuaminika ya utoaji wa oksijeni na inayofanyakazi itaokoa maisha wakati wa janga hilo la COVID-19 na kumudu kutibu wagonjwa katika siku zijazo.” 

Tathimini inasema kufuatia janga la COVID-19 nchi nyingi zimeripoti uhaba mkubwa wa oksijeni na ongezeko la bei ya huduma hiyo nan chi kama India, Bangladesh na Nigeria zimearifu idadi kubwa ya vifo vya homa ya kichomi. 

Shirika la afya ulimwenguni WHO limesema nchi masikini kabisa hivi sasa zinakadiriwa kuwa na kati ya asilimia 5 hadi 20 tu ya mahitaji ya oksijeni yanayotakiwa. 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter