Uchafuzi wa hewa wachochea nimonia: Oksijeni yahitajika

Mtoto akipokea matibabu ya oksijeni katika hospitali katika Jimbo la Bengal Magharibi nchini India.
© UNICEF/Partha Mitra
Mtoto akipokea matibabu ya oksijeni katika hospitali katika Jimbo la Bengal Magharibi nchini India.

Uchafuzi wa hewa wachochea nimonia: Oksijeni yahitajika

Afya

Kuelekea siku ya kimataifa ya kutokomeza ugonjwa wa Nimonia duniani, shirika la Umoja wa Mataifa la kufanikisha upatikanaji wa tiba nafuu UNITAID limetoa wito kwa washirika wote kuongeza kwa kasi ufadhili katika uzalishaji wa oksijeni na kujiunga na ubia wa kampeni ya  KILA PUMZI INAHESABIKA ili kuhamasisha kupunguza vifo vitokanavyo na uchafuzi wa hewa.

Kwa mujibu wa UNITAID ripoti ya mwaka 2019 inaonesha nusu ya vifo vyote vya watoto wenye umri wa chini ya mwaka mmoja katika nchi za Nigeria, India, Pakistan, Ethiopia na Niger vimesababishwa na ugonjwa mmoja wa Nimonia. 
  
Nimonia, ni ugonjwa wa kupumua unaoathiri mapafu ukisababishwa na maambukizi ya virusi, vimelea, na fangasi ambapo hata kabla ya janga la COVID-19, ulikuwa ukisababisha vifo vingi ulimwenguni. 
 
Ndio maana shirika la Umoja wa Mataifa la kufanikisha upatikanaji wa tiba nafuu, UNITAID limetoa wito kwa washirika wake katika ngazi zote, kuongeza fedha ili kupunguza vitokanavyo na nimonia kama anavyoeleza Robert Matiru, Mkurugenzi wa Programu wa shirika hilo. 

“Tunahitaji kujitolea zaidi kisiasa katika ngazi zote. Tunahitaji uwekezaji wa ziada, hasa kwa bidhaa za kiafya zinazoweza kuleta mabadiliko. Mfano vifaa vya kupima kiwango cha oksijeni kwa watoto ili kugundua magonjwa hatari na pia upatikanaji wa oksijeni yenyewe ambayo itaokoa maisha. Tunahitaji juhudi zilizoratibiwa zaidi kati ya washirika wote katika ngazi ya kimataifa, kikanda na nchi.” 
  
Na iwapo hawatafanya hivyo? “Kuna uwezekano kuwa nchi nyingi za kipato cha chini na cha kati hazitafikia malengo ya Maendeleo Endelevu yaliyowekwa kufikia mwaka 2030, ambapo ni  miaka tisa tu kutoka sasa.” 
  
Tarehe 12 ya mwezi Novemba kila mwaka ni siku ya kutokomeza Nimonia duniani, na UNITAID pamoja na kuhimiza kuongezwa kwa ufadhili, pia imehamasisha kujiunga katika kampeni ya KILA PUMZI INAHESABIKA ili kuhimiza serikali za nchi zenye idadi kubwa ya vifo kuchukua hatua ili kupunguza vifo vinavyohusiana na uchafuzi wa hewa.