Skip to main content

Wakati nakua, ukatili majumbani niliona jambo la kawaida, sasa hapana!

Livhuwani Hellen Dzibana, (kulia) akizungumza na moja ya wateja wake jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini.
UNICEF VIDEO
Livhuwani Hellen Dzibana, (kulia) akizungumza na moja ya wateja wake jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini.

Wakati nakua, ukatili majumbani niliona jambo la kawaida, sasa hapana!

Afya

Livhuwani Hellen Dzibana, mshauri nasaha kutoka nchini Afrika Kusini, kutwa kucha hivi sasa anaomba janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 limalizike kwa kuwa limekuwa mwiba katika utekelezaji wa majukumu yake kwa ufasaha ya kusaidia manusura wa ukatili wa kingono, jambo ambalo analisimamia kidete baada ya kulitambua kwa kina. Kulikoni? 
 

Livhuwani, mkazi huyu wa mji mkuu wa kibiashara wa Afrika Kusini, Johannesburg anasema kwamba katu wakati wa makuzi yake hakuwahi kufahamu maana ya ukatili wa kijinsia. John Kibego na maelezo zaidi.

Anasema, ”tuliona ukatili kama jambo la kawaida. Nilielewa kuwa mwanaume lazima awe mkuu wa familia. Lakini sasa natambua kuwa ulikuwa ni ukatili wa majumbani, ukatili wa kijinsia.”

Lakini sasa Livhuwani ni mshauri nasaha akifanya kazi yake kuwanusuru wale waliotwama kwenye ukatili wa kijinsia, lakini ujio wa COVID-19 ulitikisa kazi yake akisema,“kanuni zilitangazwa na niliamka asubuhi nikaenda ofisini kukusanya faili zangu na nikaanza kufanyia kazi nyumbani. Nilipanga upya ratiba ya wateja wang una kuwajulisha kuwa mazungumzo yetu sasa yatakuwa kwa njia ya simu. Ilikuwa kazi kubwa.”

Livhuwani Hellen Dzibana, mfanyakazi wa kijamii nchini Afrika Kusini akizungumza na mmoja wa wateja wake.
UNICEF VIDEO
Livhuwani Hellen Dzibana, mfanyakazi wa kijamii nchini Afrika Kusini akizungumza na mmoja wa wateja wake.

Tangu kuanza kwa COVID-19 tafiti iliyofanywa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF katika mataifa 104, imeonesha kuvurugwa kwa huduma zinazohusiana na msaada kwa watoto wanaokumbwa na ukatili majumbani.

Ongeko la vitendo vya ukatili linadhihirishwa na Livhuwani ambaye anasema, “kumekuwepo na visa vingi ya ukatili wa majumbani na ukatili wa kingono kutokana na vizuizi vya watu kusalia majumbani. Hali ni ngumu zaidi kwa sababu nahitaji pia kuona na kufuatilia. Kwa hiyo ni vigumu kwangu kupata taswira halisi, unafahamu mtu akizungumza amevaa barakoa ni vigumu kwangu mimi mshauri wa nasaha kuunganisha kile asemacho na anachohisi kwenye mwili wake.”

Sasa ndoto yake ni kurejea tena kwa vikao vya uso kwa uso na bila barakoa ili aweze kufanya kazi yake ipasavyo ya kunusuru wale waliotwama kwenye vitendo vya ukatili.