Alice Wairimu Nderitu wa Kenya kuwa mshauri maalum UN kuhusu kuzuia mauaji ya kimbari 

10 Novemba 2020

Katibu Mkuu wa Umoja wa MataifaAntónio Guterres leo ametangaza kumteua Alice Wairimu Nderitu kutoka Kenya kuwa mshauri maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu kuzuia mauaji ya kimbari. 

Bi. Nderitu anarith nafasi ya Adama Dieng raia wa Senegal, ambaye Katibu Mkuu amemshukuru kwa uongozi wake imara, kujitoa na mafanikio yaliyopatikana. 

Guterres pia amemshukuru Navamanee Ratna(Pramila) Patten ambaye ni mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu kuhusu ukatili wa kingono katika mizozo kwa kukaimu nafasi ya mshauri maalum kuhusu kuzuia mauaji ya kimbari . 

 

Wasifu wa Alice Nderitu 

Bi. Nderitu amekuwa ni sauti inayotambulika mashinani kwa ujenzi wa amani na kuzuia ukatili, na amewahi kuongoza na kuwa mpatanishi na mshauri wa ngazi ya juu katika mchakato wa maridhiano nchini mwake Kenya lakini pia katika maeneo mengine ya Afrika. 

Aliwahi kuhudumu kama kamishina wa tume ya kitaifa ya ushirikiano na utangamano nchini Kenya mwaka 2009-2013 na pia alikuwa mwanachama mwanzilishi na mwenyekiti mwenza wa jukwaa la Uwiano la amani, shirika la kuzuia lakini pia linalounganisha utoaji wa tahadhari ya mapema na hatua za mapema nchini Kenya. 

Bi. Nderitu pia ni mwanzilishi wa ‘Community Voices for Peace and Pluralism” mtandao wa wanawake wenye taaluma barani afrika wa kuzuia, kubadili na kutatua machafuko ya kikabila, rangi na kidini kote duniani. 

Uzowefu wake kitaifa 

Bi. Nderitu uzowefu wake kitaifa ni pamoja na kuhudumu kama mkurugenzi wa Elimu kwa ajili ya Haki Fahamu mwaka 2007-2009, mkuu wa mpango wa elimu ya haki za binadamu na kujenga uwezo  kwa ajili ya tume ya kitaifa ya haki za binadamu nchini Kenya na kamati ya haki za binadamu kati yam waka 1999-2007. 

Pia amewahi kuwa mtafiti na msimamizi wa huduma za magereza Kenya , kwenye wizara ya mambo ya ndani mwaka 1992-1999. 

Anahudumu kama mjumbe wa kamati ya kityaifa ya kuzuia na kuadhibu uhalifu wa mauaji ya kimbari, uhalifu wa vita, uhalifu dhidi ya binadamu na aina zote za ubaguzi, kwenye mtandao wa Muungano wa Afrika wa Wanawake wa Afrika katika kuzuia migogoro na upatanishi (Fem-Wise) na mtandao wa wanawake wa kupigania amani. 

Bi. Nderetu ana shahada ya uzamili ya “migogoro ya silaha na mafunzo ya amani” aliyoipata mwaka 2013 na shahada ya Sanaa, Fasihi na Falsafa aliyohitimu mwaka 1990 kutoka chou kikuu cha Nairobi. 

Ni mwanachama mshiriki wa mpito katika Taasisi ya haki na upatanisho nchini Afrika Kusini. 

Ameshaandikwa sehemu mbalimbali kutokana na taaluma na kazi zake na pia amepokea tuzo mbalimbali zinazotambua kujitolea kwake katika utatuzi wa migogoro kwa njia ya amani kote Afrika na pia kwa mbinu zake bunifu katika upatanishi. 

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter