Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mauaji ya kimbari ya Rwanda hayakuwa bahati mbaya wala yasiyoweza kuepukika:Guterres

Kumbukumbu ya Mauaji ya Kimbari ya 1994 dhidi ya Watutsi nchini Rwanda (2019).
UN Photo/Violaine Martin
Kumbukumbu ya Mauaji ya Kimbari ya 1994 dhidi ya Watutsi nchini Rwanda (2019).

Mauaji ya kimbari ya Rwanda hayakuwa bahati mbaya wala yasiyoweza kuepukika:Guterres

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema mauaji ya kimbari ya Rwanda dhidi ya Watutsi ya mwaka 1994 hayakuwa ya bahati mbaya wala yasiyoweza kuepukika.

Ameyasema hayo kupitia ujumbe wake maalum wa siku hii ya kimataifa ya kumbukizi ya mauaji hayo dhidi ya Watutsi walio wengi, wahutu wenye msimamo wa wastani na wengine waliopinga mauaji hayo.

Guterres amesema siku hii inayoadhimishwa kila mwaka Aprili 7 ni ya kuwaenzi waliipoteza maisha, kusimama pamoja na mnepo wa manusura na kutafakari kushindwa kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua kwani amesema mauji hayo. “Yalikuwa ya makusudi, yaliyopangwa na yalitekelezwa mchana kweupe. Hakuna mtu aliyefuatilia Habari za kimataifa au kutazama habari angeweza kukataa ukatili mbaya uliokuwa ukitokea. Hata hivyo ni wachache sana waliozungumza na wachache zaidi walijaribu kuingilia kati. Mengi zaidi yangeweza kufanywa na nyalipaswa kuwa yamefanywa.” 


Kwa mantiki hiyo amesema hata katika kizazi baada ya tukio hilo , doa la aibu linaendelea. Ameikumbusha dunia kwamba miaka 28 baada ya mwagaji damu huo siku zote kuna chaguo . “Kuchagua ubinadamu badala ya chuki, huruma dhidi ya ukatili, ujasiri badala ya kuridhika na upatanisho dhidi ya hasira. Kanuni za wajibu wa kulinda zinaainisha bayana kwamba hatuwezi tena kufumba macho tunaposhuhudia uhalifu wa kikatili.” 

 Guterres amesisitiza katika wito wake wa kuchukua hatua na mipango mingine, kwamba haki za binadamu husimama kidete katika kiini cha kila kitu tunachofanya. 

Aongeza kuwa mauaji ya kimbari ya Rwanda yalizusha maswali mengi na leo hii dunia inakabiliwa na mtihani mwingine , vita vya Ukraine ambako amesema kunawaka moto huku kwingineko Mashariki ya Kati na Afrika migogoro ikiendelea. 

Hivyo amesema katika siku hii “Tukijutia yaliyopita hebu tusonge mbele kwa utatuzi. Tuahidi kuwa makini na asilani kutosahau kilichotokea, na tuwaenzi kikamilifu Wanyarwanda waliopoteza maisha kwa kujenga mustkbali wenye utu, kuvumiliana na haki za binadamu kwa wote.”